Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar zimefanya kikao cha ushirikiano kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya Muungano na yasiyo ya Muungano, leo Februari 16, 2026, Zanzibar.
Kikao hicho ngazi ya Makatibu Wakuu kimepokea na kujadili taarifa ya maandalizi ya kikao maalumu cha Kamati ya Pamoja kinachotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dkt. Islam Seif Salum ambaye ni Mwenyekiti ameongoza kikao hicho pamoja na Mwenyekiti Mwenza ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Salum alisisitiza watendaji kutoka Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuendeleza ushirikiano ambao utaendelea kuimarisha Muungano.
Alisema Serikali zote mbili zinaweza kuimarisha ushirikiano huo kupitia sekta mbalimbali kwa mfano Uchumi wa Buluu ambao tayari SMZ imeanzisha Wizara mahsusi ya kusimamia na kwa upande wa SJMT Ofisi ya Makamu wa Rais ina kitengo maalumu cha usimamizi wa sekta hiyo.
“Niwaombe tu wataalamu wenzetu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar tuendeleze ushirikiano katika Sekta ya Uchumi wa Buluu ili kuona namna gani utanufaisha wananchi,” alisema.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Mitawi alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza mazungumzo na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano ili kupata fungu maalum ambalo litasaidia kuhakikisha na kuwezesha utoaji wa elimu maalumu kuhusu Muungano.
Alisema suala la utoaji wa elimu ni la kimkakati hivyo, nguvu kubwa imewekezwa katika kuhakikisha mkazo unatiliwa katika utoaji wa elimu ili kutowapa nafasi wapotoshaji wa Muungano.
Bw. Mitawi pia, alitoa wito kwa watendaji kutoka pande zote mbili za Muungano kutanua wigo wa ushirikiano kwa kuzungumzia agenda zingine zinazogusa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Sio mbaya tukiwa na watu wa Manunuzi na idara mbalimbali kama Utumishi, Sheria, Mazingira na Uchumi wa Buluu mkikutana na kuzungumzia fursa zenu au changamoto zenu na kushirikiana katika kuzifanyia kazi,” alisema.
Katika kikao hicho wajumbe wamepokea taarifa ya Mpango Kabambe wa Elimu kwa Umma kuhusu Muungano ambao utatumika katika kuelimisha wananchi kuhusu historia, misingi, faida na fursa mbalimbali za Muungano.
Sanjari na hilo pia, iliwasilishwa tarifa ya maendeleo ya mifumo ikiwemo Mfumo wa Uratibu wa Shughuli za Serikali na Mfumo wa uratibu wa Masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kikao cha ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ngazi ya Mawaziri.








