





………………………………
OFISI ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kampuni ya Tulive Private Equity Limited ya Namibia zimetiliana saini hati ya mashirikiano (MoU) katika kuanzisha utaratibu wa kusimamia biashara ya kaboni kwa sekta za usafiri wa anga na bahari katika Mamlaka ya Zanzibar.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Migombani, Mjini Unguja, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maryam Juma Abdalla, alisema makubaliano hayo yanalenga kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa fedha za kaboni utakaojumuisha ukusanyaji na usimamizi wa michango ya fedha kutoka kwa vyombo vya usafiri vinavyochangia uzalishaji wa gesi chafuzi visiwani humo.
“Zanzibar itaanzisha mfumo rasmi wa usajili, ufuatiliaji na usimamizi wa taarifa za fedha zinazohusiana na uzalishaji wa hewa ukaa (carbon emissions) zinazotokana na ndege na meli zinazoachilia hewa chafu (rejista). Mfumo huu utahakikisha kila fedha inayokusanywa inarejeshwa hapa na kutumika katika miradi ya maendeleo na uhifadhi wa mazingira,” alisema Maryam.
Alibainisha kuwa mfumo huo utasaidia upatikanaji wa rasilimali zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira, ikiwemo nishati jadidifu, usafiri rafiki kwa mazingira, uhifadhi wa mikoko na misitu, usimamizi wa taka, pamoja na miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mapema, Katibu Maryam alieleza kuwa mfumo rasmi wa kupima, kufuatilia, kuripoti na kuhesabu uzalishaji wa gesi joto (GHG) unaotokana na shughuli za usafiri wa anga na bahari nchini utasaidia kuimarisha juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa msingi wa kimazingira wa “anayesababisha uchafuzi hulipa” (polluter pay principle), mhusika atawajibika kufidia gharama za kuzuia, kudhibiti na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
“Kutokana na makubaliano haya, ndege na meli zitakazothibitika kuchangia uzalishaji wa hewa chafu zitachangia fedha kama sehemu ya fidia ya athari za mazingira, ambapo fedha hizo zitarejeshwa Zanzibar na kuelekezwa katika miradi ya maendeleo na uhifadhi wa mazingira,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA), Sheha Mjaja Juma, alisema Zanzibar ni miongoni mwa maeneo yanayoathirika moja kwa moja na ongezeko la joto duniani, kupanda kwa kina cha bahari na mabadiliko yasiyotabirika ya mifumo ya mvua, licha ya kuwa si mzalishaji mkubwa wa gesi chafuzi.
“Makubaliano haya yatatuwezesha kuingia rasmi katika mfumo wa ufuatiliaji wa hewa ukaa (carbon emissions), kujua kiwango cha uzalishaji kinachotokana na safari za ndege na meli zinazoingia na kutoka Zanzibar, na hatimaye kupata mgao wetu stahiki,” alisema Mjaja.
Alifafanua kuwa kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikipokea idadi kubwa ya ndege na meli za kimataifa, lakini haikunufaika moja kwa moja na michango ya kifedha inayotokana na hewa chafu wanayoizalisha.
Hivyo, kupitia makubaliano hayo, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaweza kufuatilia chombo kilichotoka, kwa mfano Japan au Ulaya, kubaini kiwango cha uzalishaji wa moshi kilichotolewa, kiasi kilicholipwa kama kodi ya kaboni na sehemu ya Zanzibar katika mgawanyo huo.
Mjaja aliongeza kuwa hatua hiyo inaendana na makubaliano ya kimataifa ya Paris Agreement yaliyofikiwa mwaka 2015, yanayozitaka nchi, mashirika na kampuni zinazochangia uchafuzi wa hewa kuchukua wajibu wa kifedha katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Zanzibar, kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni mshiriki wa makubaliano hayo.
Alisema tayari Zanzibar ina Sheria ya Mazingira ya mwaka 2015 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 kuruhusu kutungwa kwa kanuni za kusimamia biashara ya kaboni, ambapo mwaka 2025 kanuni hizo zilitungwa rasmi kutoa mwongozo wa namna biashara ya kaboni itakavyofanyika na mgao utakavyopangwa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Tulive Private Equity Limited, Arthur Katsvara, alisema lengo la mpango huo ni kusaidia nchi za Afrika kuhakikisha fedha za kodi ya kaboni zinazokusanywa kutokana na shughuli za usafiri wa anga na majini zinarejeshwa katika nchi husika badala ya kubaki nje.
“Kodi yoyote ya kaboni inayokusanywa kutokana na safari za ndege au meli zinazohusiana na Zanzibar inapaswa kurejeshwa hapa. Rejista ndiyo chombo cha kuhakikisha ukusanyaji na urejeshaji huo unafanyika kwa uwazi na uwajibikaji,” alisema.
Aliongeza kuwa fedha zitakazokusanywa zitatumika katika miradi rafiki kwa mazingira, ikiwemo uzalishaji wa nishati safi, upatikanaji wa maji safi na salama, miradi ya kupunguza uchafuzi wa maji, pamoja na miradi mingine ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kuhusu changamoto za kifedha, alisema nchi nyingi za Afrika zimekuwa na sera na sheria bora za mazingira, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha. Kupitia mfumo huo, Serikali haitalazimika kutoa fedha kuanzisha rejista, bali gharama zitaendeshwa kupitia makusanyo ya kodi ya kaboni.
Aidha, alibainisha kuwa wakaguzi huru watakuwepo kuhakikisha fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa kuzingatia vipaumbele vitakavyowekwa na Serikali ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi, alisema suala la kaboni lina uhusiano wa karibu na sekta ya nishati na kueleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yameathiri vyanzo vya jadi vya uzalishaji umeme, hususan maji, kutokana na vipindi virefu vya ukame.
“Ni lazima tuhamie katika suluhisho la nishati jadidifu kama umeme wa jua na upepo ili kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kujenga mfumo imara wa nishati,” alisema.
Alisisitiza kuwa ingawa Zanzibar haina viwanda vikubwa vinavyochafua hewa, bado inaathirika na uchafuzi unaotokana na mataifa mengine, hali inayofanya mpango huo kuwa wa kimkakati katika kulinda maslahi ya wananchi na mazingira ya visiwa hivyo.
Kupitia makubaliano hayo, Zanzibar inaelekea kuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza barani Afrika kuanzisha mfumo mahsusi wa kurejesha mapato ya kodi ya kaboni yanayotokana na usafiri wa anga na majini, hatua inayotarajiwa kuimarisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.


