Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nicholas Livingstone, Februari 26, 2026 amefungua rasmi mafunzo maalum ya siku tatu kwa askari wa usalama barabarani pamoja na madereva, yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali.
Mafunzo hayo yatafanyika katika ukumbi wa Vwawa, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe ambayo yamewajumuisha wakuu wa vikosi vya usalama barabarani kutoka Mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa.
ACP Livingstone, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Jeshi la Polisi wa kuongeza ufanisi kazini na kuimarisha utendaji wa askari wa kikosi cha usalama barabarani katika kusimamia sheria za usalama barabarani.
Aidha, ACP Livingstone aliwataka askari hao kukemea na kuchukua hatua kwa vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni za Jeshi la Polisi, huku akiwasisitiza umuhimu wa askari kuwa na weledi, nidhamu na kutumia lugha nzuri wanapotoa huduma kwa wananchi, ili kujenga imani kwa jamii na kuhakikisha haki inatendeka kwa wote bila upendeleo.
Mafunzo hayo yatatolewa siku 03 yakiongozwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Mwashamba Onesmo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Tanzania, ambayo yamelenga kuwajengea uwezo askari wa vikosi vya usalama barabarani kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuhusu mifumo mbalimbali ya kiutendaji pamoja na nguzo muhimu za kuwa dereva bora.
Katika siku hizo za mafunzo hayo yatawahusisha wadau wa usafirishaji na wamiliki wa vyombo vya moto, ikiwemo wamiliki wa shule za udereva, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa usalama barabarani na uzingatiaji wa sheria, ili kupunguza ajali na kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.









