Na Mwamvia Mwinyi, JamhiriMedia, Pwano
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Pwani inakuja na utaratibu mpya kwa wafanyabiashara wa mafuta katika Bandari ya Bagamoyo wanaosafirisha bidhaa hiyo kutoka Zanzibar, hatua itakayoanza kutekelezwa kuanzia Machi, 2026 kwa lengo la kuboresha ukusanyaji kodi ulio rafiki kwa wafanyabiashara hao.
Aidha, mamlaka hiyo imekanusha taarifa za kufungwa kwa bandari hiyo na kuwataka wachukuzi, wafanyabiashara na wananchi kupuuza propaganda zinazosambazwa.

Akitoa ufafanuzi kuhusu utaratibu huo katika mkutano wa wafanyabiashara wa mafuta, wajasiriamali na wachukuzi uliofanyika Februari 27, 2026, Meneja wa TRA Pwani, Masawa Masawa, alisema kwa niaba ya Kamishna Mkuu kuwa lengo la serikali ni kujenga mazingira rafiki ya biashara sambamba na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato.
Alieleza dhamira ya serikali ni kuona wafanyabiashara wanatimiza wajibu wao bila kutumia njia za panya kuingiza bidhaa kwa kukwepa ushuru au kodi, hali inayoweza kuhatarisha afya za walaji na kudhoofisha ushindani wa kibiashara.
“TRA haijafunga bandari, Changamoto ilijitokeza baada ya wafanyabiashara kutoa malalamikia mbalimbali, serikali iliunda timu ya kufuatilia na kupata suluhisho la moja kwa moja, na kazi hiyo imekamilika,” alibainisha Masawa.

Aliongeza kuwa kuanzia mwezi Machi 2026, utaratibu huo mpya utaanza rasmi kutumika na utakuwa nafuu zaidi kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga alieleza kuwa bandari hiyo ni kitovu muhimu cha ajira ambapo takribani vijana 400 wanategemea shughuli mbalimbali za kiuchumi, na kusimama kwa biashara hiyo kuliathiri kipato na zoezi la usajili wafanyabiashara.
Ndemanga aliishukuru serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali na kuimarisha mazingira ya biashara.
Meneja Msaidizi ,Forodha na Ushuru wa Bidhaa mkoani Pwani, Melinda Matinyi alieleza ,wafanyabiashara hao ni muhimu kwani wanachangia mapato ya serikali kwani ulipaji kodi ni muhimu.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Shaban Hamsini, alielezea kuzorota na kusuasua kwa shughuli bandarini kuliathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa wafanyabiashara na mapato ya halmashauri .

Diwani wa Kata ya Dunda, Amir Mpwimbwi, alifafanua asilimia 80 ya eneo la bahari lipo katika kata hiyo, hivyo wananchi wengi hutegemea shughuli za baharini kujipatia kipato.
Aliishukuru serikali kwa kushughulikia changamoto hiyo na kueleza matumaini kuwa uchumi wa eneo hilo utarejea katika hali yake ya kawaida .
Mchukuzi wa madumu ya mafuta, Wema Abdallah, alisema wamechoka kukaa bila kazi kwa zaidi ya miezi miwili, hali iliyowakosesha kipato cha kujikimu.






