Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKOA wa Pwani unaungana na mikoa mingine nchini kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, huku kilele cha maadhimisho kimkoa kikitarajiwa kufanyika Machi 8, 2026 katika Uwanja wa Ujamaa, Kata ya Umwe, Tarafa ya Ikwiriri, Halmashauri ya Mji Rufiji.
Mratibu wa maadhimisho hayo mkoani humo, Roseline Kimaro, amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Ameeleza, maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Haki kwa Wanawake na Wasichana, Msingi wa Maendeleo Jumuishi Dira 2050,” inayosisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na ulinzi wa haki za wanawake na wasichana.
Kimaro amebainisha kwamba, maadhimisho hayo pia yanatoa fursa ya kuhamasisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kilele cha maadhimisho hayo.





