Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Rais wa Kenya, William Samoei Ruto, amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda wakati akihitimisha kipindi chake cha uenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza katika mkutano wa 25 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha, Tanzania, Ruto amesema katika mwaka mmoja wa uongozi wake, nchi wanachama zimeendelea kuimarisha mshikamano na ushirikiano unaolenga ustawi wa wananchi wa kanda hiyo.
Ruto alieleza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imeendelea kujidhihirisha kama moja ya jumuiya za kikanda zenye nguvu na matarajio makubwa barani Afrika kutokana na juhudi za pamoja za viongozi wa nchi wanachama.

Amesema dira ya pamoja ya kanda hiyo inayolenga ustawi wa wananchi, amani na mshikamano imeendelea kuongoza juhudi za nchi wanachama katika kukuza maendeleo ya pamoja ya kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Ruto, katika kipindi chake cha uenyekiti kumekuwapo hatua muhimu katika kuimarisha nguzo kuu za jumuiya hiyo ikiwamo ujumuishaji wa kiuchumi, usalama wa kikanda, maendeleo ya miundombinu na ushirikiano unaowalenga wananchi moja kwa moja.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa Muungano wa Forodha na Soko la Pamoja umeendelea kuimarishwa huku hatua zaidi zikichukuliwa kuelekea kufikiwa kwa Muungano wa Fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.
Kuhusu masuala ya usalama, Ruto amesema amani na utulivu wa kikanda ni msingi muhimu wa maendeleo ya kanda hiyo, akipongeza juhudi za nchi wanachama kushirikiana kukabiliana na changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa kisiasa, mazungumzo na hatua za pamoja zimeongeza uwezo wa nchi wanachama kulinda amani na kuhakikisha usalama wa wananchi wa Afrika Mashariki.

Ruto pia amegusia umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kikanda ikiwamo barabara, reli, bandari, nishati na miundombinu ya kidijitali ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa kanda hiyo.
Amesema miundombinu bora inachangia kurahisisha biashara ya kikanda, kuvutia uwekezaji na kuunda ajira kwa vijana ambao ni kundi kubwa la watu katika nchi za Afrika Mashariki.
Aidha, amekiri kuwa licha ya kukua kwa biashara ndani ya kanda, bado kuna haja ya kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru na kurahisisha taratibu za mipakani ili kuongeza ufanisi wa soko la kikanda.
Ameongeza kuwa hatua hizo zitasaidia kuimarisha viwanda vya ndani, kuwapa nguvu wafanyabiashara wa ndani na kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika Mashariki katika soko la kimataifa.
Katika hotuba yake, Ruto pia alisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu ambazo zinaathiri uchumi na maisha ya wananchi wa kanda hiyo.

Akihitimisha hotuba yake, Ruto ameishukuru Sekretarieti ya EAC na taasisi zake kwa mchango wao katika kusukuma mbele ajenda ya jumuiya hiyo, akieleza imani yake kuwa kwa mshikamano na ushirikiano wa dhati, Afrika Mashariki itaendelea kujenga kanda yenye amani, ustawi na maendeleo kwa wananchi wake.



