*Vijana waapa kuonyesha maajabu
*Watoa kongole kwa Rais Samia

Na Byarugaba Innocent OR-MV, Mwanza

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe.Joel Arthur Nanauka leo Machi 7, 2026 amezindua program ya Jenga Kesho iliyobora (BBT) upande wa uvuvi kwa kuwakabidhi hundi yenye thamani ya Bilioni 7 Vijana 308 wanaojishughulisha na Mambo ya uvuvi ili iwawezeshe kimitaji hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya chuo cha uvuvi (FETA) kilichopo Nyegezi Jijini Mwanza

Mhe.Nanauka amemshukuru na Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake ya kutoa bilioni 200 kwa ajili ya Vijana ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeshapokea bilioni 30 kati ya 200 kutekeleza fursa zinazoibuliwa na Vijana kwenye Sekta ya Mifugo na uvuvi

Mhe.Nanauka amewahakikishia Watanzania kuwa utoaji wa hundi ya Bilioni 7 kwa Vijana hao 308 wa Mikoa ya Mwanza,Mara na Kagera ni Mwanzo wa Safari ya kuwathibitishia Watanzania kuwa uwekezaji kwa Vijana una tija na Taifa linatarajia nidhamu, weledi, ubunifu na uwajibikaji katika kutekeleza Miradi inayoibuliwa na Vijana wenyewe.

Aidha,Mhe.Nanauka ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Waziri Dkt.Bashiru Ally Kakurwa na Naibu Mhe.Ngw’asi Kamani kuwa Wizara kinara kwa tukio la linalofanyika la utoaji wa hundi ya Bilioni 7 kwani ni utekelezaji kwa vitendo ahadi za Rais Samia alizozitoa wakati wa kampeni.

Mhe.Nanauka ametumia fursa hiyo kuwatoa hofu Vijana kuhusu fedha hizo kwa kuhofia masharti magumu kwani kwa sasa hakuna Kijana atakosa mikopo kwa kukosa sifa na kwamba hayo ni Maelekezo ya Rais Samia na kwamba anayekosa sifa asaidiwe na wataalam kuzipata sifa stahiki.


“..Hakuna dhamana yoyote inayohitajika, unaweza kupata mkopo hata ukiwa peke yako, Kuna muda wa matazamio kati ya miezi 3-8 baada ya kuanza Miradi wako, Kuna Mafunzo kabla ya kuanza kazi na Walezi wa kuwaongoza tumefanya hivi ili kila Kijana kushiriki Kujenga uchumi wa Taifa” …amesema Nanauka

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi,Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe.Ngw’asi Kamani amesema utekelezaji wa program hiyo umepitia hatua tatu; kuandaa Mafunzo kwa Vijana ya kuwabadili mtazamo uliojengeka wa kuajiriwa badala ya kutumia fursa zilizopo kijiajiari pamoja na kutumia ujuzi walionao,Kutoa Mafunzo kwa vitendo na uatamizi yaliyolenga kukuza ujuzi hasa kwenye ukuzaji viumbe Maji na uwezeshaji kimitaji ili waweze kutekeleza Miradi waliyoibuni wakiwa mafunzoni.

Naibu Katibu Mkuu-Uvuvi Prof. Mohamed Shekhe ameeleza kuwa Vijana 308 kati ya Vijana 486 waliopata Mafunzo miaka 3 iliyopita wanakwenda kutekeleza Miradi ya uvuvi, Ufugaji Samaki kwa njia ya Vizimba kwenye Ziwa Viktoria,Unenepeshaji wa Majongoo na Kaa pamoja na kilimo cha Mwani.

Amesema kuwa Vizimba vilivyozinduliwa vinauwezo wa kuweka vifaranga 11,500 vinavyoweza kufikisha tani 3.5 kwa kizimba baada ya miezi 7 kwa gharama ya Shilingi 17,246,188 ambapo wa kiuzwa kwa bei ya Shilingi 7,500 kwa kila kilo moja ya Samaki wanaweza kufikisha Shilingi 26,500,000 na kuzalisha faida ya Shilingi 9,003,811 kwa mzunguko.

Erasto Bukeyedeo na Grace Henry Wanufaikaji wa bilioni 7 wamemshuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka Vijana na kutoa bilioni 200 na kwamba kwa Miradi wanayokwenda kutekeleza inakwenda kutoa ushuhuda kuwa Vijana wakiaminiwa, wanaweza hivyo wameahidi kujituma ili kuzalisha kwa tija.