Rais wa Iran ameomba radhi kwa kuyashambulia mataifa ya kikanda, lakini ameendelea kuikosoa Marekani. Kauli yake imekuja wakati makombora na droni za Iran vikiendelea kuruka kuelekea Israel na mataifa ya Ghuba ya Kiarabu.

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ametupilia mbali madai ya Marekani ya kujisalimisha bila masharti siku ya Jumamosi, huku akiomba radhi kwa mashambulizi ya Iran dhidi ya nchi za eneo hilo, wakati Israel na Marekani zikiendelea na mashambulizi yao ya anga dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Nchi za Ghuba zilisema zimefanikiwa kuzuia makombora zaidi ya balistiki na droni zilizorushwa kutoka Iran.

Saudi Arabia ilisema ilizuwia droni nne zilizokuwa ziaelekea kushambulia uwanja mkubwa wa mafuta wa Shaybah, ikiwa ni shambulio la pili ndani ya saa chache. Ndege zinazoingia na kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai zilisitishwa baada ya abiria kupelekwa kwenye mahandaki ya treni huku milipuko kadhaa ikisikika na tahadhari kutangazwa.

Wakati huo huo, ndege za kivita za Israel zimeshambulia kwa nguvu miji ya Beirut na Tehran. Idadi ya vifo imeendelea kuongezeka Jumamosi huku watu takribani 1,230 wakiuawa Iran, zaidi ya 200 Lebanon na takriban watu kumi na wawili Israel, kulingana na maafisa. Wanajeshi sita wa Marekani pia waliripotiwa kuuawa.