Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wakikabiliwa na tuhuma za rushwa na uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAKUKURU, washtakiwa hao ni Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Abdallah Mohamed Jaha, pamoja na Mhasibu wa halmashauri hiyo, Rajabu Diamond Mushi, ambao wanakabiliwa na kesi namba 5949/2026 inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Godfrey Haule.
TAKUKURU imeeleza kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa matatu, likiwemo matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na kifungu cha 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (R.E 2022).
Aidha, taasisi hiyo imeongeza kuwa washtakiwa wanadaiwa pia kuisababishia Serikali hasara kinyume na masharti ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022.
“Katika kipindi cha kuanzia Machi 2, 2024 hadi Juni 30, 2024, washtakiwa walijihusisha na udanganyifu katika mchakato wa manunuzi kwa kutumia nyaraka zilizoonesha kuwa mbao aina ya marine boards 692 zilipokelewa kutoka SAIFI STORE, jambo lililopelekea kufanyika kwa malipo ya shilingi 83,528,073,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya TAKUKURU.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi umebaini kuwa mbao zilizowasilishwa zilikuwa 500 pekee, hali iliyopelekea upotevu wa fedha za umma.
TAKUKURU imefafanua kuwa washtakiwa walinuia kujipatia manufaa ya shilingi 7,810,560, kiasi ambacho pia kimeisababishia Halmashauri ya Wilaya ya Muheza hasara ya kiwango hicho.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na kwa sasa wapo nje kwa dhamana huku kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Muheza.


