Wakati vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran vikiingia siku yake ya 28 siku ya Ijumaa, kunatajwa dalili za mazungumzo ya kukomesha vita hivyo, ingawa mashambulizi baina yao hayajasita.

Iran na Marekani bado zipo njia panda kuhusu suala zima la kumaliza vita vya Mashariki ya Kati huku kila upande ukionekana kusalia na msimamo wake kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano, jambo linalotishia mzozo huu kuongezeka hasa ikiarifiwa kuwa maelfu ya wanajeshi wa Marekani wanakaribia eneo hilo.

Hata hivyo, mjumbe maalum wa rais wa Marekani Steve Witkoff amesema kuna “ishara za wazi” kuwa Tehran wako tayari kujadiliana , huku shirika la habari la Iran Tasnim likiripoti kuwa jibu la Iran kwa pendekezo la Marekani lilitumwa rasmi jana usiku kupitia wapatanishi, na kwamba kwa sasa Tehran inasubiri jibu.

Afisa wa Iran ambaye hakutaka kutajwa jina amesema miongoni mwa mashari ya Iran ni kudai fidia kutokana na uharibifu uliosababishwa na vita na kwamba uhuru wa Iran kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz ni lazima uheshimiwe, matakwa ambayo amesema hayakuwemo kwenye mpango huo wa Marekani.