Wanajeshi 12 wa Marekani wamejeruhiwa kufuatia shambulio lililolenga kambi ya anga ya Prince Sultan nchini Saudi Arabia, huku vita kati ya Iran na Marekani na Israel ikiingia mwezi wa pili.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka 10 iliyoripotiwa awali, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani.

Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kuwa wanajeshi hao walijeruhiwa katika shambulio la Iran lililohusisha angalau kombora moja pamoja na ndege zisizo na rubani (drones), kwa mujibu wa mshirika wa habari wa BBC, CBS.

Inaelezwa kuwa angalau wanajeshi wawili wako katika hali mbaya sana baada ya jengo walilokuwwepo ndani kulengwa moja kwa moja wakati wa shambulio hilo.

Vyanzo visivyotajwa vimeeleza kuwa pia ndege kadhaa za kujaza mafuta angani ziliharibiwa katika tukio hilo.

Hadi wakati wa kuripoti habari hii, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) pamoja na Kamandi Kuu ya Marekani (US Central Command) hazikuwa zimetoa tamko rasmi kujibu taarifa hizo.