Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa
Siku za hivi karibuni kumekuwa na taharuki zilizosababisha vurugu na kukosekana kwa amani na utulivu wa jamii katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Rukwa. Hali hii ilisababishwa na watu kuzusha kuibiwa nyeti zao.
Kufuatia taharuki hizo kuzuka, Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa tarehe 06 Aprili 2026, lilifanya msako na kufanikiwa kuwakamata vijana saba (07) Wilaya ya Sumbawanga waliodai kuwa wameibiwa nyeti zao. Vitendo hivyo vilichochea wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia watu wasio na hatia.
Vijana wawili kati ya hao saba ambao ni Haruni Willium Mengo (24), Mkazi wa Kalambazite na Isack Simon Kaniki (19),Mkazi wa Mshani wamefikishwa Mahakamani na kuonekana na hatia. Wote wawili wamepewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miezi sita (06) jela kila mmoja. Adhabu hiyo imetolewa Aprili 08,2026 na Mh. Wiligisi Mbunda hakimu wa Mahakama ya mwanzo Kipeta Wilaya ya Sumbawanga. Ni kuwa tarehe 06/04/2026 wakiwa kijiji cha Mshani Wilaya Sumbawanga vijana hao walimzushia Issa Athumani Kidungwe (56), mkazi wa Handeni Tanga kuwa ameiba nyeti zao, hivyo alishambuliwa kwa kupigwa maeneo mbalimbali ya mwili kitendo kilichomsababishia maumivu mwilini.
Watuhumiwa wengine watano (05) wanaendelea kushikiliwa. Nao ni: Geofrey Milumba Deminic (24), Jafari Nebart Shanjila (25) wakazi wa kijiji cha Kilangawana, Huruma Geofrey Kasonso (18), Mkazi wa Kilyamatundu, Costantino Octavian Kiatu (28) na Severino Cosmas Ngonyani (22), Wakazi wa Sumbawanga. Taratibu za kuwafikisha mahakamani zinakamilishwa.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha tabia inayoendelea ya kuzusha taharuki. Pia wananchi wanasisitizwa kutojichukulia sheria mkononi, na kwamba wote wanaotuhumiwa wafikishwe Polisi ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Vilelevile wananchi wanahimizwa kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi pale wanapobaini viashiria vya vurugu au uhalifu.


