Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TANZANIA bado inachangia chini ya asilimia moja ya mabaharia duniani, hali inayofungua fursa kubwa kwa sekta binafsi kuongeza juhudi za kuzalisha mabaharia wengi wenye ujuzi.

Imeelezwa hatua hiyo itasaidia kufanikisha malengo ya maendeleo ya sekta hiyo kuelekea Tanzania Development Vision 2025.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam Maritine Training Academic (DTMA), Kapteni Ken Chimwejo wakati wa ufunguzi wa chuo cha kwanza binafsi cha mafunzo ya ubaharia nchini.

“Tanzania bado tuko katika kuchangia idadi kubwa ya mabaharia, nazisihi mno sekta binafsi kuongeza juhudi za kuzalisha mabaharia wengi zaidi na wenye ujuzi ili kushindana na mataifa mengine ulimwenguni.

“Tumefungua chuo hiki ili kuwezesha vijana wetu wapata elimu na mafunzo ya kina ambayo yatawasaidia kujiajiri kokote duniani, chuo hiki kitajikita kuwajengea uwezo vijanazania ili wakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa katika taaluma ya ubaharia,”amesema.

Amesema juhudi hizo zinaungwa mkono na Tanzania Shipping Agencies Corporation (TASAC) ambayo inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kukuza taaluma ya ubaharia nchini.

Amesema kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya ubaharia duniani, nchi ya Philippines inaongoza kwa kutoa zaidi ya asilimia 25 ya mabaharia duniani, huku ripoti zikionyesha mwaka 2026, dunia inakabiliwa na upungufu wa takribani asilimia 86 ya mabaharia.

Amesema Tanzania bado ina upungufu mkubwa wa mabaharia, jambo linaloonyesha kuwa kuna fursa kubwa kwa vijana kujiunga na taaluma hiyo.

Amesema ekta ya ubaharia ina mchango mkubwa katika uchumi wa dunia, kwani takribani asilimia 90 ya bidhaa zote duniani husafirishwa kupitia njia za maji, hivyo kuifanya kuwa sekta yenye nafasi kubwa ya ajira kwa vijana.
Amesema chuo hicho kinakuwa kwanza binafsi kutambuliwa, kuthibitishwa rasmi na kusajiliwa kutoa elimu na mafunzo ya ubaharia kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Mafanikio haya yamefikiwa baada ya mamlaka za Serikali zenye dhamana ya kusimamia elimu nchini kufanya kaguzi za kina chuoni kuona miundombinu, vifaa vya kufundishia, mitaala, sifa za wakufunzi pamoja na mifumo ya usimamizi na uendeshaji, na kujiridhisha kwamba chuo kinakidhi viwango vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa.

Amesema mafunzo ya msingi yanajumuisha kozi mbalimbali zinazotolewa ni mbinu binafsi za kujiokoa baharini, kuzuia na kupambana na moto,mafunzo ya huduma ya kwanza, usalama binafsi,wajibu kwa wenzako na mafunzo ya uelewa ya ulinzi baharini.

“Mafunzo yanalenga kumwandaa mhitimu aweze kumudu mazingira ya kazi za bahari, kumjengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za bahari na kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa umahiri na weledi,”amesema.