Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Zaidi ya ajira 50,000 zimezalishwa kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini, hatua inayoonesha mchango mkubwa wa miradi hiyo katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Takwimu hizo zimewasilishwa bungeni Aprili 9, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini),Rahma Kisuo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,Jasmine Chesco kuhusu nafasi za ajira kwa vijana kwenye miradi mikubwa.
Akifafanua, amesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) umeongoza kwa kutoa ajira zaidi ya 35,000, ukifuatiwa na mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) uliotoa ajira zaidi ya 10,000.
Ameongeza kuwa sekta ya miundombinu pia imechangia ajira hizo ambapo zaidi ya watu 2,400 wamepata ajira kupitia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Kwa upande wa miradi mingine, daraja la Kigongo–Busisi limetoa ajira zaidi ya 1,500 huku upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam ukizalisha ajira zaidi ya 3,000.
Mbali na ajira, Serikali pia inaendelea kuwawezesha vijana kupata ujuzi kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ili waweze kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati na sekta ya viwanda.
Amesema hatua hiyo inaendana na utekelezaji wa sera na sheria mbalimbali za kitaifa zinazolenga kukuza ajira na ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa nchi.



