Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 09 Aprili 2026 alipokutana na ujumbe wa wataalamu kutoka Shirika la Afya Duniani, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Afrika, Profesa. Mohamed Yakub Janabi, waliowasili Ikulu Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia WHO kuwa Serikali imekuwa ikifanya juhudi za makusudi kuhakikisha inaendelea kutumia rasilimali za ndani kukabiliana na changamoto za kiafya, huku ikiendelea kutafuta wadau na washirika wa maendeleo wa kimataifa ili kuimarisha sekta hiyo.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kudhibiti na kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza (NCDs), kuimarisha afya ya uzazi kwa mama na mtoto, pamoja na kuwajengea uwezo wauguzi wa ngazi ya jamii kupitia mafunzo, ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya sekta ya afya.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Profesa. Mohamed Yakub Janabi, amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya ili kufikia malengo na vipaumbele vyake, hususan katika kudhibiti maradhi mbalimbali.
Wataalamu hao wa WHO wamesifu hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuelekeza bajeti yake ya ndani katika kuimarisha sekta za afya, elimu na huduma za kijamii, wakieleza kuwa ni mfano bora kwa nchi nyingine nyingi za Kanda ya Afrika.











