Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Mabalozi walioteuliwa kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi kuhakikisha wanaangalia furasa za biashara na uwekezaji ambazo Tanzania inaweza kufaidika nazo.

Akizungumza ofisi kwake Vuga alipokuwa akiagana na mabalozi hao, Mhe. Hemed amewataka kulinda maslahi ya Tanzania, kuimarisha Uchumi na biashara kwa kuzitangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Amesema lengo la kuteuliwa kwao ni kwenda kuiwakilisha Tanzania na watazania wote hivyo ni vyema kuhakikisha wanaimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na nchi wanazoziwakiliksha ili kulinda hadhi na heshima ya Tanzania.

Amewataka kwenda kuangalia fursa zilzopo katika nchi zao ambazo zinaweza kuisaidia Tanzania katika kupiga hatua kimaendeleo ikiwemo suala zima la biasha na uwekezaji.

Akitoa shukurani kwa niaba ya mabalozi wenzake, Balozi CYPRIAN JOHN LUHEMEJA wa Zambia amesema watahakikisha wanafanya kazi zao kwa ushirikiano na uweledi mkubwa kwa kufuata maelekezo na miongozo wanayopatiwa na Viongozi wakuu wa nchi.

Mabalozi walioagwa ni Balozi Mhandisi Zena Ahmed Said ( Saudi Arabia ), Balozi Cyprian John Luhemeja ( Zambia ), Balozi Maulidah Bwanaheri Hassan ( Oman ), Balozi Salim Othman Hamad ( Comoros ), Balozi Swahiba Habib Mndeme ( Sweden ), Balozi Noel Emmanuel Kaganda ( Korea ) na Balozi Mussa Haji Ali, Naibu Mwakilishi wa Kudumu Umoja wa Mataifa, New York.