Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetangaza hatua mpya ya kuboresha utoaji huduma kwa kuunganisha mifumo ya kidijitali ya TANCIS ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na RIMS ya TMDA, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kasi katika uingizaji wa bidhaa za afya nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo amesema kuwa muunganiko huo utawezesha wadau kutumia mfumo mmoja wa TANCIS katika kuwasilisha maombi ya vibali na kufanya utambuzi wa mizigo, badala ya kutumia mifumo miwili tofauti kama ilivyokuwa awali.
Amesema kuanzia Mei 1, 2026, waingizaji wote wa mizigo mikubwa ya forodha ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi watalazimika kuwasilisha maombi yao moja kwa moja kupitia mfumo wa TANCIS, jambo litakalorahisisha michakato na kupunguza urasimu.
“Lengo kuu ni kuwa na sehemu moja ya kuingiza taarifa, kuboresha ufuatiliaji wa maombi pamoja na kuimarisha udhibiti wa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini kwa njia ya kielektroniki,” amesema Dk. Fimbo.
Katika hatua hiyo, TMDA imewataka waingizaji kuhakikisha wanazingatia usahihi wa taarifa za bidhaa, ikiwemo namba za usajili na taarifa za majengo, ili kuepusha ucheleweshaji au hoja zisizo za lazima wakati wa ukaguzi.
Aidha, wadau wametakiwa kushirikiana kwa karibu na mawakala wa forodha ili kuhakikisha nyaraka zote za kitaalam zinakidhi vigezo vinavyohitajika kabla ya kuwasilishwa kwenye mfumo.
TMDA imefafanua kuwa mabadiliko hayo yanawahusu waingizaji wa mizigo mikubwa ya forodha pekee, na hayahusu wale wanaoingiza bidhaa kwa matumizi binafsi.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za umma, sambamba na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta ya afya.



