OFISI za Gazeti la Pambazuko linalosambazwa kila wiki, zimevunjwa na kuibwa kwa nyaraka, laptop mbili na kamera.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo – Aprili 10, 2026 kwenye ofisi zake zilizopo kwenye Jengo la Pambazuko lililoko Mtaa wa Mpakani A, Kijitonyama, Kinondoni, Dar es Salaam.
Tayari uongozi wa gazeti hilo umeripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi Mabatini – Kijitonyama na maofisa wa jeshi hilo wameanza uchunguzi wa tukio hilo huku wakilipa namba ya uchunguzi; KJT/RB/13172026.

Jengo hilo lenye kamera za kufuatilia matukio, lina walinzi wawili wa usiku na mmoja wa mchana, lakini hadi sasa mlinzi mmoja amekamatwa na anaendelea kuhojiwa na vyombo vya usalama.
Vifaa vilivyoibwa, vimesababisha matayarisho ya kuzalisha gazeti kusimama kwa sasa na juhudi zinaendelea kuhakikisha matayarisho ya kuandaa Pambazuko yanaendelea.
Mhariri Mkuu wa Pambazuko, Simon Mkina alipoulizwa endapo anahisi tukio linahusiana na kuminywa kwa uhuru wa habari alisema hana uhakika kuibwa kwa vifaa hivyo kunahusiana na kazi za kutafuta, kuchakata, na kusambaza gazeri hilo, licha ya Tanzania kuwa katika mtanziko wa uhuru wa habari nchini.
Mkina anasema kamera za kufuatilia matukio kwenye ofisi hizo kwa sasa zinachunguza zaidi na kwamba taarifa zitatolewa kadri zinavyopatikana.







