Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dododoma
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamehimizwa kupunguza matumizi ya karatasi na kutimia mfumo wa kidijitali katika shughuli za Bunge ili kukabiliana na changamoto ya uchafuzi wa mazingira.
Wito huo umetolewa bungeni jijini Dodoma na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu wakati akiongoza cha Kikao cha Bunge leo Aprili 10, 2026.
Alisema kuwa mojawapo ya shughuli zinazochangia uchafuzi wa mazingira ni pamoja na matumizi makubwa ya karatasi hivyo kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa.
“Bado kuna Waheshimiwa Wabunge wanaomba kuchangia kwa kutumia karatasi, hizi karatasi zinachafua mazingira kwenye nchi yetu, kwahiyo niwaombe sana mtumie mfumo huu ni rahisi sana,” alisisitiza Mhe. Zungu.
Aidha, ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira tayari Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na taasisi mbalimbali imeendelea kuchukua hatua madhubuti zikiwemo kutumia mifumo mbalimbali ya mtandao katika katika utendaji.
Mifumo ya mtandao inawezesha utekelezaji wa shughuli za Serikali zikiwemo za Bunge kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hivyo kurahisisha utendaji na kupunguza matumizi ya karatasi.
Matumizi ya TEHAMA kwa kiasi kikubwa yamepunguza kutumia karatasi ambazo matumizi yake yakiisha kama zisipodhibitiwa hugeuka taka na hivyo kuchafua mazingira.







