Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 30 mnyamwezi, mkulima, mkazi wa maeneo ya Cheyo-A, Kata ya Cheyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora amejichoma kisu tumboni kwa hasira baada ya kugombana na mpenzi wake.

Akizungumzia tukio jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Richard Abwao ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Aprili 7 mwaka huu majira ya saa 9 alasiri huko maeneo ya Cheyo A katika Kata ya Cheyo.

Ameeleza kuwa mwanamke huyo baada ya kugombana na mwenzake, kwa hasira aliamua kuchukua kisu na kujaribu kujiua kwa kujichoma tumboni hali iliyosababisha sehemu ya utumbo wake kutoka nje.

Kamanda amefafanua chanzo cha tukio hilo kuwa ni wivu wa kimapenzi baina ya dada huyo na mpenzi wake mwenye umri wa miaka 33 Mngoni, mkazi wa Cheyo anayefanya kazi ya bodaboda.

Amebainisha kuwa tukio hilo ni la pili kwa dada huyo, kwani tukio la kwanza (huko nyuma) aliwahi kujirusha juu ya ukuta kwa hasira na kuvunjika mguu wake wa kulia, baada ya kutoelewana na mpenzi wake huyo.

‘Kwa sasa mtuhumiwa amepewa PF 3 na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi wa afya yake, baada ya hapo hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,’ ameeleza.

Kamanda Abwao ametoa wito kwa jamii kuacha kuchukua maamuzi hatarishi kama hayo kwa kuwa yanawaingiza kwenye matatizo na kuwataka kutoa taarifa za migogoro ya kifamilia kwenye mamlaka husika ikiwemo kutumia Dawati la Jinsia.

Amesisitiza kuwa kujaribu kujiua ni kosa kisheria, na kuongeza kuwa inapotokea wapenzi wawili hawaelewani hilo linaamuliwa kwa kukaa pamoja kwenye Ofisi zinazohusika ili kupata ufumbuzi kwa amani na siyo kujiua.