Tanzania na Belarus zimekubaliana kupanua wigo wa ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kiteknolojia katika sekta mbalimbali za maendeleo zenye maslahi ya pamoja.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Belarus,Mhe. Maxim Ryzhenkov, uliofanyika Aprili 28, 2026 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kombo amesema pande hizo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za kilimo, nishati, afya, elimu na miundombinu kwa kutumia teknolojia za kisasa na kubadilishana uzoefu, hatua inayolenga kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kupunguza urasimu pamoja na kuimarisha mifumo ya utekelezaji wa miradi ya pamoja katika sekta husika, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, kuvutia uwekezaji zaidi na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya pande zote.
Kwa upande wake, Mhe.Ryzhenkov amesema Belarus iko tayari kushirikiana na Tanzania bega kwa bega katika sekta hizo, akisisitiza dhamira ya kuongeza uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya nchi hizo mbili.















