Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea

Wahitimu wa Chuo cha Ualimu Songea kilichopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wametakiwa kuongeza juhudi katika kujifunza na kufundisha masomo ya sayansi ili kusaidia azma ya Tanzania ya kuwa nchi ya viwanda.

Akizungumza katika mahafali ya saba ya kuhitimisha mafunzo ya ualimu ngazi ya Stashahada maalum ya chuo hicho, mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Nemacha General Business Martin ambaye aliwakilishwa na mfanyabiashara Meck Mguhi amesema kuwa walimu wa sayansi wana nafasi kubwa katika kujenga msingi imara wa elimu utakaowezesha kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali za viwanda na teknolojia.

Ameeleza kuwa maendeleo ya viwanda hayawezi kufikiwa bila kuwa na rasilimali watu yenye ujuzi wa kutosha katika sayansi na ubunifu, akibainisha kuwa walimu ndio chachu ya mabadiliko hayo kuanzia ngazi za chini za elimu.

“Tunawahitaji walimu wenye uwezo wa kufundisha sayansi kwa vitendo na kwa ubunifu ili kuwajengea wanafunzi hamasa ya kujifunza na kufanya tafiti,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Catherine Kimboka amesema kuwa chuo cha Ualimu Songea ni miongoni mwa Vyuo 34 vya Serikali vinavyotoa mafunzo ya Ualimu ngazi ya Stashahada Maalum ambayo hutolewa kwa miaka mitatu na kwamba mara baada ya Kumaliza hupangiwa kazi katika shule za Sekondari kote nchini.

Amesema kuwa chuo hicho kimeendelea kupata sifa nzuri ya kitaaluma na kitaalam kutokana na matokea mazuri ya mitihani ya kitaifa kwa muda wa miaka mitatu.

Kimboka ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan kuwaletea fedha za ukarabati wa baadhi ya majengo chuoni hapo huku akitumia kauli ya kushukuru ni kuomba tena ameiomba Serikali kuwaletea fedha kwaajiri ya kumalizia ukarabati wa majengo yaliyobaki pamoja na miundo mbinu ya maji taka.

Akisoma risala ya wahitimu ya Stashahada Maalum ya Ualimu Sekondari katika mahafari ya 07 Ramadhan Mlanga alisema kuwa walianza mafunzo wakiwa Jumla ya wanafunzi 144 kati yao wakike 36 na wakiume 108 ambapo hadi wanahitimu wapo wanafunzi 106 wakike 23 na wakiume 83 aidha 36 waliacha kwa sababu mbali mbali.

Aidha wamewashukuru walimu pamoja na uongozi wa chuo ukiongozwa na mkuu wa chuo hicho Kimboka katika kipindi chote walichokaa chuoni hapo na kuweza kupewa mafunzo na utaalam katika tasnia mbali mbali ikiwemo taaluma katika masomo ya Baiolojia,fizikia Kemis,Hisabati na TEHAMA pamoja na utaalam katika masomo ya Ualimu na kufanya mafunzo kwa vitendo.