Na Mwandishi Wetu, Tanga

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati katika kulinda maisha ya wafanyakazi, baada ya kufikia zaidi ya saa milioni sita za kazi bila kurekodi ajali yoyote kazini.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi yaliyofanyika Chongoleani mkoani Tanga, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa EACOP, Bw. Paul Hiegel, alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji thabiti wa kauli mbiu ya “Zero Harm” (Hakuna Madhara Sehemu ya Kazi).

Alisema mradi huo unaweka usalama kuwa kipaumbele cha kwanza kwa kuhakikisha kila mfanyakazi anatekeleza majukumu yake katika mazingira salama.


“Tunajivunia kuona wafanyakazi wetu wanarudi nyumbani salama na kuungana na familia zao wakiwa na furaha,” alisema Bw. Hiegel.

Aliongeza kuwa usalama si tukio la siku moja, bali ni utamaduni unaojengwa kila siku. Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu, “Mind on Target, Eyes on Target,” EACOP inalenga kuongeza umakini wa wafanyakazi katika akili na macho yao katika kutambua na kuepuka hatari.


“Tunataka kila mfanyakazi arejee nyumbani akiwa salama, bila majeraha yoyote,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wafanyakazi wote kuzingatia matumizi ya vifaa vya kujikinga (PPE) muda wote wanapokuwa kazini, akieleza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kujilinda na kulinda wengine.

Kwa upande wake, Mkuu Msaidizi wa Kambi ya MTT ( Marine Tanks Terminal) kunakojengwa miundombinu ya kuhifadhi mafuta ghafi katika Pwani ya Chongoleani mkoani Tanga, Bw. Jerome Betat, alisema mradi huo unahusisha wafanyakazi kutoka mataifa mbalimbali, hivyo usalama wao ni jambo la msingi hadi wanaporejea salama nyumbani baada ya kukamilika kwa mradi.

Alieleza kuwa EACOP imewekeza katika mafunzo ya mara kwa mara na mifumo madhubuti ya usalama ili kupunguza hatari kazini.

Naye Meneja wa Usalama wa Afya na Mazingira, Bi. Stay Bidgewater, alisema maadhimisho ya siku hiyo ni fursa muhimu ya kuwakumbusha wafanyakazi wajibu wao katika kudumisha usalama.


Aliongeza kuwa huu ni mwaka wa tano kwa mradi huo kuadhimisha siku hiyo tangu ulipoanza.

Bi. Bidgewater alibainisha kuwa wafanyakazi wanaruhusiwa kusimamisha kazi mara moja wanapoona hatari yoyote, bila kusubiri ruhusa kutoka kwa wasimamizi.
“Lengo ni kuzuia ajali kabla hazijatokea,” alisema.

Aliongeza kuwa kupitia kampeni ya “Zero Harm,”, mradi huo hutoa zawadi kila mwezi kwa wafanyakazi wanaochangia kuzuia ajali, hatua inayosaidia kupunguza gharama za matibabu na kuongeza ufanisi kazini.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bw. Salum Inegeja, aliipongeza EACOP kwa juhudi zake za kuhakikisha wafanyakazi wanazingatia matumizi ya vifaa vya kujikinga kama inavyotakiwa kisheria.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa EACOP, Bi Catherine Mbatia alisema maadhimisho hayo yanaonesha dhamira ya mradi huo katika kuweka usalama mbele.


“Lengo ni kuhakikisha kila mfanyakazi anakuja kazini salama na kurejea nyumbani salama,” alisema.

Aliongeza kuwa wafanyakazi wanahimizwa kutoa taarifa za hatari mapema, huku kila siku kabla ya kuanza kazi wakifanya tathmini ya shughuli za siku iliyopita ili kuboresha usalama zaidi.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo ya uendeshaji mitambo, Bw. Sifa Obadia, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu umuhimu wa usalama kazini.
“Tunazingatia usalama ili kuhakikisha hakuna madhara kwa watu wala miundombinu,” alisema.

Mradi wa EACOP unamilikiwa na kampuni ya TotalEnergies kwa asilimia 62, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Mafuta la Uganda (UNOC) kila moja likimiliki asilimia 15, na kampuni ya CNOOC ya China ikimiliki asilimia 8.

Baadhi ya wafanyakazi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) wakiadhimisha Siku ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi kwa kukumbushana matumizi ya vifaa vya kujikinga (PPE) wakati wote wanapokuwa kazini. Hafla hiyo fupi ilifanyika jana katika eneo la mradi, Chongoleani mkoani Tanga.