Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kwa miongo minne imefanikiwa kutoa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), kwa miradi 35,000 hatua iliyowezesha uwekezaji kufanyika kwa uwajibikaji mkubwa zaidi.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo, Dk Immaculate Semesi, wakati akizungumzia miaka 40 ya NEMC na safari ya Tanzania kuelekea mustakabali wa kijani na maendeleo endelevu.
Dk Semesi alisema hiyo si takwimu tu bali ni ni ushahidi wa namna Tanzania ilivyofanikiwa kuoanisha ukuaji wa uchumi na ulinzi wa mazingira.
Alisema katika sekta ya viwanda na biashara, utoaji wa vibali zaidi ya 28,000 umeimarisha uzingatiaji wa viwango vya mazingira, hivyo kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Aidha, alisema juhudi za kudhibiti uchafuzi wa mazingira zimeokoa taifa gharama kubwa ambazo zingetumika kurekebisha madhara ya kimazingira na kiafya.
“Uwekezaji katika maarifa nao haujaachwa nyuma kwani kupitia mafunzo na miongozo, wataalamu zaidi ya 12,000 wamejengewa uwezo, wakisambaza utaalamu huo katika taasisi za serikali, sekta binafsi na vyuo vya elimu ya juu,” alisema.
Alisema katika dunia inayokabiliwa na changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la uchafuzi wa mazingira na kupungua kwa rasilimali asilia, hadithi ya Tanzania inajitokeza kama mfano wa matumaini, uthabiti na maamuzi ya kimkakati.
Alisema maadhimisho ya miaka 40 ya (NEMC) si tukio la kawaida bali ni kielelezo cha dhamira ya Taifa kulinda uhai wake huku likiendeleza uchumi wake.
Alisema kuanzishwa kwa NEMC mwaka 1986 kulikuja katika kipindi ambacho dunia ilikuwa inaanza kutambua kwa kina uhusiano kati ya mazingira na maendeleo.
Alisema Tanzania, kwa maono ya mbali, iliweka msingi wa taasisi itakayokuwa mlezi wa rasilimali zake kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema mara nyingi mjadala wa mazingira huwekwa kando kana kwamba ni suala la pembeni lakini ukweli ni kwamba mazingira ndiyo msingi wa uchumi wa Tanzania.
Dk Semesi alisema kilimo, ambacho kinaajiri sehemu kubwa ya Watanzania, kinategemea afya ya udongo na upatikanaji wa maji na kwamba utalii, sekta muhimu ya mapato ya kigeni, unategemea uwepo wa bioanuai na mifumo hai ya ikolojia.
Aidha, alisema misitu ya Tanzania, inayochukua zaidi ya nusu ya eneo la nchi, si tu makazi ya viumbe hai bali pia ni hifadhi kubwa ya hewa ukaa (carbon sink).
Alisema pamoja na mafanikio hayo, changamoto bado ni kubwa kwani kila mwaka, Tanzania inapoteza maelfu ya hekta za misitu kutokana na shughuli za kibinadamu kama ukataji miti holela, kilimo kisicho endelevu na matumizi ya nishati isiyo rafiki kwa mazingira.
Aliongeza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, mafuriko na mabadiliko ya mifumo ya mvua—zinaendelea kuathiri maisha ya wananchi na sekta za uzalishaji.
“Hizi ni changamoto zinazohitaji zaidi ya sera zinahitaji mabadiliko ya mtazamo, teknolojia bunifu, na ushirikiano mpana wa wadau wote.
Alitaja moja ya mafanikio makubwa ya NEMC kuwa ni kuhamasisha ushiriki mpana wa wadau katika uhifadhi wa mazingira na kwamba wananchi zaidi ya milioni 4.2 wamefikiwa na elimu ya mazingira—hatua inayojenga kizazi chenye uelewa na uwajibikaji.
“Sekta binafsi nayo imeanza kuchukua nafasi muhimu kupitia uwekezaji katika teknolojia safi, urejelezaji na uzalishaji unaozingatia mazingira. Huu ni mwelekeo sahihi kuelekea uchumi wa kijani (green economy),” alisema.
Alisema katika kuelekea kilele cha maadhimisho tarehe 29 Mei 2026, shughuli kama upandaji wa miti 40,000, utoaji wa elimu kwa maelfu ya wadau, na majadiliano ya kitaifa kuhusu mustakabali wa mazingira zinaashiria mwelekeo mpya wa hatua za vitendo.
“Huu ni wakati wa kujiuliza: Je, tunataka kuacha urithi gani, je tunataka vizazi vijavyo vikute misitu au jangwa, mito yenye uhai au mito iliyokauka,” alihoji Dk Semesi
Alisema safari ya miaka 40 ya NEMC inaonesha wazi kuwa Tanzania ina uwezo wa kuwa kinara wa maendeleo endelevu kwani mafanikio ya kesho yatategemea maamuzi ya leo.
“Kila Mtanzania ana jukumu: kupanda mti, kupunguza uchafuzi, kutumia rasilimali kwa busara, na kuhamasisha wengine kufanya hivyo kwani kwa pamoja, tunaweza kujenga taifa lenye mazingira salama, uchumi imara, na maisha bora kwa wote,” alisema.



