Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali kwa kufanya doria za kubaini na kuzuia uhalifu.
Pia oparesheni na misako imeendelea kufanyika na kufanikiwa kuwakamata wahalifu waliotenda uhalifu.
Watuhumiwa waliokamatwa na upelelezi kukamilishwa walifikishwa Mahakamani na baadhi wamepatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo.
Katika Mahakama ya Wilaya ya Kyela Zawadi Jackson Mwakijolo, Mwandishi wa habari na mtangazaji wa kituo cha 94.1 Keifo Fm, Mkazi wa Itunge Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya amepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 60 jela kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi vifurushi 142 vyenye uzito wa kilo 155.84.
Hukumu hiyo imetolewa na Mhe. Paul Mabula Barnabas Aprili 29, 2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Kyela. Imeelezwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo tarehe 2.2.2025 na alikamatwa na Askari akiwa anasafirisha dawa hizo kutokea katika kivuko kisicho rasmi cha January kwa ajili ya kupeleka maeneo mbalimbali ya nchi kufanya biashara hiyo haramu.
Mshitakiwa ametiwa hatiani na kuhukumiwa kwa mujibu wa Sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Aidha, Yesaya Watson Mwakyoma, Mkazi wa Kafundo Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya katika Mahakama hiyo hiyo ya Wilaya ya Kyela amepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka alilolitenda dhidi ya mtoto mwenye umri wa miaka 7 ambaye ni Mwanafunzi wa Darasa la Pili.
Hukumu hiyo imetolewa na Mhe. Paul Barnabas Aprili 29, 2026. Kabla ya hukumu hiyo ilielezwa kuwa Mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 10, 2025 baada ya kumkuta mtoto huyo akiwa anacheza na watoto wenzake katika makazi ya mtuhumiwa kisha kumshika mkono na kuingia naye chumbani kwake na kumwingilia kimwili.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali Wakili Brice Kessi (SA) akiwa mahakamani hapo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe funzo kwa watu wengine wenye tabia kama hizo ili kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto katika jamii.
Imetolewa na:
Kaimu Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya



