Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limewakamata watu wawili kwa tuhuma za kuwafanyia ukatili wa kinyama watoto kwa kuwachoma moto na kuwasababishia majeraha na maumivu makali.

Watuhumiwa hao ni Fortunatus Benezet Mawela (60), mkazi wa kijiji cha Singiwe Wilaya ya Kalambo, na Aisha Credo Mpepo (25), mkazi wa kitongoji cha Kasanzama, mji mdogo wa Laela wilaya ya Sumbawanga.

Fortunatus Benezet Mawela alimchoma moto mjukuu wake wa kiume miaka (16) tumboni na mapajani huku akiwa amemfunga mikono na miguu akimtuhumu kumuibia ndizi Aprili 19, 2026.

Tarehe 27 Aprili 2026 Aisha Credo Mpepo alimuunguza mgongoni mtoto wake wa kiume miaka (8) kwa kutumia pasi ya umeme baada ya kumtuhumu mtoto wake huyo kumuibia shilingi 2,000 aliyopanga kununulia mkaa.

Taratibu zinakamilishwa ili watuhumiwa hao wawili waweze kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo za kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto hao.

Vilevile Mahakama ya Wilaya ya Kalambo imemhukumu Bosco John Fatachi (38), mkazi wa Kijiji cha Kambo, wilaya ya Kalambo kulipa faini ya shilingi 300,000 au kwenda jela miaka mitatu.

Adhabu hiyo imetolewa baada ya mahakama kuridhika kwamba mshtakiwa alimuadhibu mtoto wa miaka (8) kikatili kwa kumpiga akitumia waya wa umeme na akiwa amemfunga kamba mikono na miguu akimtuhumu kumuibia pipi zenye thamani ya shilingi 200 dukani kwake.

Hakimu Nickson Temu iliamuru mshitakiwa amlipe mtoto huyo fidia ya shilingi 500,000 huku akisisitiza iwe ni fundisho kwa watu wote wenye tabia za kuwafanyia ukatili watoto.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linaendelea kulaani vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na linatoa wito kwa wazazi na walezi kuacha kutoa adhabu za kikatili kwa watoto badala yake wawape malezi yaliyo bora. Pia Jeshi la Polisi linawapongeza na kuwashukuru wananchi wanaotoa taarifa za kufichua vitendo vya ukatili majumbani.