WAZIRI MKUU Dk. Mwigulu Nchemba amesema vyombo moto vinavyotumika katika kujipatia kipato vikiwemo pikipiki na bajaji visishikiliwe kwa makosa madogo pale mhusika anapotambulika badala yake viachwe kwa wahusika ili wavifanyie kazi na kupata fedha za kulipa faini.

Mheshimiwa Waziri Mkuu amefafanua kwamba vyombo hivyo ni vile ambayo vimekamatwa kwa makosa yasiyohusisha uhalifu wa kutumia silaha, dawa za kulevya au mauaji na kwamba agizo hilo lisitafsiriwe kama ruhusa ya kuvunja sheria za usalama barabarani.

Ameyasema hayo leo Alhamisi, Aprili 30, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali ipo tayari kupitia upya utaratibu wa kukamatwa na tozo za vyombo vya moto.

“Makosa madogo ambayo yanahusisha faini hakuna ulazima wa kushikilia chombo ikiwa muhusika anatambulika kisheria kwa sababu Watanzania wengi wana vitambulisho vya Taifa na vyombo hivyo vinausajili, hivyo wahusika waelekezwe kulipa faini na waachiwe vyombo na kuendelea kujitafutia kipato”.

Pia, Waziri Mkuu amesisitiza kwamba lengo la Serikali la kutoza faini si kutumia kama chanzo cha mapato bali ni kurekebisha nidhamu na kuimarisha usalama barabarani kwani tayari Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alishaelekeza faini zipitiwe upya baada ya kubainika baadhi yake zilikuwa kubwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za ucheleweshaji wa upelelezi wa mashauri ya jinai ili watuhumiwa wajue hatima yao kwa wakati.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Doto Bahemu, aliyetaka kujua kwa nini baadhi ya kesi zimekua zikichukua muda mrefu kufanyiwa uchunguzi na kutolewa maamuzi, wakati nyingine huamuliwa kwa haraka.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema malalamiko hayo yalifikishwa pia kwenye Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo tayari iliwasilisha mapendekezo yake Serikalini na tayari yameanza kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kutenganisha makosa madogo na makubwa ili kurahisisha uchunguzi.

Waziri Mkuu amesema pia, Serikali imeanza kufanya maboresho ya mifumo ya haki jinai kwa kuunganisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Mahakama, Polisi na Magereza kidijitali ili mafaili yasitembee tena kwa mkono. “Hili litapunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki,” alisema.