*Ni kipindi cha mwezi Julai 2025 hadi Machi 2026, Watanzania 19,695 waajiriwa katika migodi
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanikiwa kuwasilisha Mipango 1,082 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akiwasilisha Bungeni makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Waziri Mavunde alilieleza Bunge kuwa, Mipango 1,081 iliidhinishwa na Mpango mmoja (1) haukuidhinishwa kutokana na kutokidhi matakwa ya Kisheria na Kanuni.
Mavunde aliongeza kuwa , Kati ya Mipango 1,082 iliyowasilishwa, 13 ilihusisha leseni za Uchimbaji Mkubwa (SML), 15 leseni za Uchimbaji Wa Kati (ML), 11 leseni za Uchimbaji Mdogo (PML), 31 leseni za Utafutaji (PL) na 1,012 ni watoa huduma mbalimbali kwa wamiliki wa leseni za madini.
Akielezea kuhusu utekelezaji wa matakwa ya Kanuni za Ushiriki wa Watanzani katika rasilimali za ndani (Local Content) Waziri Mavunde alilieleza Bunge kuwa, Tume ya Madini ilitangaza huduma na bidhaa 20 ambazo zinapaswa kutolewa na watanzania au kampuni zinazomilikiwa na watanzania ambapo hadi kufikia Machi 2026, jumla ya ajira 20,421 zilizalishwa katika migodi mbalimbali.
“Ni vyema ikafahamika kwamba kati ya ajira hizo, idadi ya watanzania 19,695 waliajiriwa na wageni 726, huku kampuni za madini na watoa huduma mgodini zilifanikiwa kununua bidhaa na kutoa huduma zenye thamani ya shilingi trilioni 4.9 ambayo sawa na asilimia 90.18 kutuoka kampuni za Tanzania” alisema Waziri Mavunde
Kwa upande wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) Waziri Mavunde alibainisha kuwa, miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 16.52 ilitekelezwa katika Mikoa ya Kimadini ikiwemo Kahama, Mara, Geita, Songwe, Singida, Dar es Salaam, Lindi, Mwanza na Shinyanga.
Miradi hiyo ilihusisha sekta ya afya, kilimo, michezo, miundombinu ya barabara, mazingira na elimu.
Kwa upande wa ukaguzi migodi, katika kipindi cha mwezi Julai 2025 hadi Machi 2026, Tume ya Madini ilifanikiwa kufanya ukaguzi wa migodi mikubwa sita (6), migodi ya kati 31 na migodi midogo 9,080 katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa 30 ya kimadini na kubaini masuala mbalimbali yasiyokidhi vigezo ikiwa pamoja na kukosekana kwa Mpango wa Ufungaji mgodi uliohuishwa.
Mapungufu mengine ni kutotekelezwa kikamilifu kwa matakwa ya Sheria ya Baruti, kukosekana kwa taarifa za usanifu wa maeneo ya kuhifadhi miambataka pamoja na mabwawa ya topetaka, kukosekana kwa meneja mgodi aliyeteuliwa kwa mujibu wa utaratibu, maduara kutokuwa na miundombinu ya kiusalama na vifaa kinga kutotumiwa ipasavyo.





