Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC) na Idara ya Habari Maelezo, wanaandaa mwongozo kwa ajili ya watengeneza maudhui katika maeneo ya jamii za pembezoni.

Mwongozo huo, unatarajiwa kuwasaidia Wanahabari na Watengeneza maudhui, kutambua maadili na miiko ya jamii za pembezoni za Wahadzabe, Masai, Datoga na Akie, kabla ya kuandika na kusambaza maudhui kuhusiana na jamii hizo.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Taasisi ya MAIPAC, Mussa Juma alitoa taarifa hiyo, jana wakati akizungumza katika mjadala wa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo Duniani (WPFD) jijini Arusha, kuhusiana na waandaaji wa maudhui mitandaoni na matumizi ya akili Unde katika kuboresha kazi zao.

Juma alisema katika katika siku za karibuni wameibuka watengeneza maudhui wa ndani nan je ya nchi, Kwenda moja kwa moja katika maeneo ya jamii hizo hasa Wahadzabe na kutoa maudhui yao bila ridhaa yao na maudhui mengine ambayo ni kinyume cha maadili.

“Kutokana na changamoto hii, MAIPAC kwa kushirikiana na UNESCO na Idara ya Habari Maelezo wanaandaa mwongozo maalum wa kufanyakazi katika jamii hizi kwa kuzingatia maadili na bila kudhalilisha utu wa jamii hizi”alisema

Alisema sambamba na mradi huo, pia MAIPAC kwa kushirikiana na UNESCO ,MAELEZO na SAVVY Media, wanatarajia kusaidia jamii hizi kujua matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii lakini pia kuanza kunufaika na matangazo na Habari ambazo zimekuwa zikitangazwa.

“Tutazijengea uwezo jamii hizi, kuweza kutumia vizuri mitandao kwa manufaa yao pia kiuchumi na kutambua haki zao mbali mbali za kidigitali na hivyo kuinua Uchumi wao”alisema

Wakizungumza katika mjadala huo, baadhi ya watengeneza maudhui mitandaoni na maafisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),walisema matumizi ya mitandao na akili unde vinapaswa kusaidia vijana na jamii badala ya kuopogwa.

Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe katika eneo la bonde la Eyasi, wilaya ya Karatu, Mdindi Samboga alishukuru MAIPAC,UNESCO,Maelezo na SAVVY Media, kuja na mradi wa kuwasaidia.

Samboga alisema jamii yao imepata umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijamii katika siku za karibuni lakini hata hivyo hainufaiki na wanaotengeneza picha na Habari.

“Wanakuja wanatupiga picha na kutuhoji tunasikia mijini tunaonekana sana lakini sisi hatunufaiki zaidi ya kupewa pombe, sasa tunaomba kusaidiwa kunufaika”alisema.