Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imepanga kuanza awamu ya pili ya kampeni ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia itakayofanyika kuanzia Mei 1 hadi 15, 2026 katika Mkoa wa Dodoma, kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuimarisha upatikanaji wa haki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 29 ,2016 Jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha wananchi hususan makundi yenye uhitaji wanapata huduma za kisheria kwa urahisi na bila gharama.

Amesema makundi yatakayolengwa zaidi ni wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana, ambao mara nyingi hukumbana na changamoto ya kupata haki kutokana na ukosefu wa huduma za kisheria.

Amefafanua kuwa katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo mwaka 2023 ,Jumla ya wananchi 86,947 mkoani Dodoma walifikiwa na huduma za msaada wa kisheria huku kati yao wanaume wakiwa 42,298 na wanawake 44,649.

“Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa migogoro 818 ilipokelewa, ambapo migogoro 452 ilitatuliwa na mingine 366 ikiendelea kushughulikiwa, ” ameeleza Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma.

Amesema katika utekelezaji wa awamu ya pili, huduma zitakazotolewa ni pamoja na ushauri wa kisheria, elimu ya sheria kwa jamii, uandaaji wa nyaraka mbalimbali za kisheria, uwakilishi mahakamani na kwenye mabaraza, pamoja na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.

Huduma nyingine ni usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, elimu kwa umma itatolewa kuanzia ngazi ya wilaya hadi vijiji na mitaa, sambamba na kufanyika katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya wananchi kama masoko, vituo vya mabasi na taasisi za elimu ili kuhakikisha ujumbe unawafikia wananchi wengi zaidi.

“Vituo vya huduma vitaanzishwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma, zikiwemo Jiji la Dodoma, Chamwino, Kongwa, Mpwapwa, Bahi, Chemba pamoja na Kondoa Mji na Kondoa Wilaya, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo katika maeneo mbalimbali, ” amesema

Aidha Senyamule amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na kampeni hiyo, akisisitiza kuwa haki ni msingi wa maendeleo ya jamii na kila mwananchi anapaswa kupata ulinzi wa haki zake.

Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,” ikiwa inalenga kuhamasisha jamii yenye usawa, haki na ustawi kwa wote kulingana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.