Na John I Bera
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), Shaikha Nasser Al Nowais, tarehe 29 Aprili, 2026 katika eneo la Victoria Falls, ambako ulikuwa unafanyika Mkutano wa Pili wa Kikanda wa UN Tourism kuhusu uwezeshaji wa wanawake katika sekta ya utalii barani Afrika.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kijaji amempongeza Bi. Al Nowais kwa kuchaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo, na kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na UN Tourism katika kukuza sekta ya utalii. Aidha, ameangazia mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo nchini Tanzania na namna yanavyoendelea kuchangia ukuaji wa uchumi.
Akizungumzia maandalizi ya AFCON 2027, Dkt. Kijaji ametumia fursa hiyo kumualika rasmi Katibu Mkuu kushiriki na kushuhudia mashindano hayo yatakayofanyika Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania huku akiliomba shirika hilo kuipatia Tanzania msaada wa kitaalam, hususan katika matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi katika kuitangaza nchi kimataifa wakati wa tukio hilo kubwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Kijaji amemjulisha Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa World Travel Awards 2026 itakayofanyika mwezi Desemba mwaka huu ambapo ametumia fursa hiyo kumualika kama mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu huyo Bi. Shaikha Al Nowais, ameahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika kuyatekeleza mambo mbalimbali ya kiutalii
Awali Dkt. Kijaji pia ameshiriki katika shughuli zinazoendelea katika mkutano huo ambao umefunguliwa rasmi na Mke wa Rais wa Zimbabwe, Auxillia Mnangagwa, ikiwemo mdahalo wa Mawaziri wa Utalii uliofanyika baada ya ufunguzi.




