Na Mwandishi Wetu
Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay unatarajiwa kuchochea kwa kiasi kikubwa biashara ya mafuta katika ukanda wa Kusini na kufungua njia mpya za usafirishaji wa bidhaa hiyo kuelekea nchi jirani kupitia miundombinu ya kisasa inayojengwa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo, Meneja wa Mipango ya Mafuta wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Gilbert Jungulu, amesema mradi huo una nafasi ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usambazaji wa mafuta kwa nchi za Malawi, Msumbiji na maeneo mengine ya ukanda huo.
Amesema PBPA itaendelea kuratibu uagizaji wa mafuta nchini pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha miundombinu muhimu ya mafuta, ikiwemo maghala ya kuhifadhia mafuta, inajengwa na kuimarishwa ili kurahisisha biashara ya kikanda.
“Endapo maghala ya kuhifadhia mafuta yatakamilika hapa Mbamba Bay, itakuwa rahisi meli kushusha mafuta kwa ajili ya kuhifadhiwa na baadaye kusafirishwa kwenda nchi jirani. Hii itaongeza matumizi ya bandari na kufungua fursa kubwa za kiuchumi,” amesema Jungulu.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo utaongeza mapato ya Serikali kupitia huduma za bandari, kuchochea shughuli za usafirishaji na kuongeza ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Agathon Mwenda, amesema bandari inajengwa kwa kiwango cha kisasa ikiwa na uwezo wa kuhudumia magari na mizigo kwa wakati mmoja, pamoja na kupokea meli zenye uwezo wa kubeba hadi tani 5,000.
Amesema matumizi ya Bandari ya Mbamba Bay yatapunguza gharama na muda wa usafirishaji wa mafuta kwenda nchi jirani, ukilinganisha na njia za sasa zinazotumia barabara kupitia maeneo mengine ya mipakani.
“Badala ya magari kuzunguka umbali mrefu kupitia Kasumulu, sasa yataweza kutumia njia hii moja kwa moja kwenda Malawi. Hii itarahisisha biashara na kuongeza ufanisi wa bandari,” amesema Mwenda.
Kwa sasa, ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay umefikia asilimia 49, hatua inayoashiria maendeleo ya mradi huo kuelekea kuwa lango muhimu la biashara ya mafuta na bidhaa nyingine kwa nchi za Kusini mwa Afrika.




