Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imesema inaendelea kuweka na kutekeleza mikakati madhubuti ya kulinda watoto walio katika mazingira hatarishi nchini sambamba na kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali ili washiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akijibu maswali bungeni Mei 22, 2026, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Maryprisca Mahundi amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya malezi, ulinzi na usalama wa watoto kupitia programu na sera mbalimbali ikiwemo Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (MTAKUWWA II 2024/25–2028/29).
Amesema mpango huo umekuwa ukilenga makundi maalum ya watoto wakiwemo yatima, wenye ulemavu pamoja na wale wanaoishi na kufanya kazi mitaani, ambao mara nyingi hukumbwa na changamoto za ukosefu wa huduma za msingi na usalama.
“Kupitia utekelezaji wa MTAKUWWA II, Serikali imeendelea kuboresha huduma za ulinzi na malezi kwa watoto nchini,” amesema Mahundi.
Kwa mujibu wa takwimu alizotoa bungeni, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara imesajili jumla ya makao ya watoto 29 na kuhuisha leseni za makao 39 yenye watoto 855. Hali hiyo imefanya jumla ya makao ya watoto kufikia 433 yanayohudumia watoto 16,130 nchini.
Aidha, vituo 809 vya kulelea watoto wadogo mchana vimesajiliwa na vinaendelea kutoa huduma kwa watoto 27,270 nchini, hatua inayoonesha ongezeko la huduma za ustawi wa jamii katika ngazi ya jamii.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mahsusi kukabiliana na changamoto ya watoto wanaolala katika stendi za mabasi na maeneo mengine ya mijini, ambapo madawati 14 ya huduma za ustawi wa jamii yameanzishwa katika vituo vya usafirishaji nchini.
Naibu Waziri huyo amesema kupitia madawati hayo, maafisa ustawi wa jamii wamekuwa wakiwafuatilia watoto hao kwa kuwahoji, kupata taarifa zao na kuwasiliana na wazazi au ndugu zao, ili kuhakikisha wanarejeshwa katika familia zao na kupata malezi stahiki.
Katika upande wa uchumi jumuishi, Mahundi amesisitiza kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika nguzo ya uchumi imara, shindani na jumuishi pamoja na nguzo ya maendeleo ya watu na jamii.
Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kiuchumi, ujuzi na mazingira bora ya kukuza biashara zao ili kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.



