Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar 3s Salaam

Umoja wa Mawakala wa Meli Tanzania (TASAA), umeeleza kuwa tozo ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (PID) ni muhimu ili kujenga miundombinu itakayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye bandari kubwa na za kisasa.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TASAA, Abel Uronu ameeleza kuwa tozo hiyo ambayo hivi karibuni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliipunguza kutoka asilimia 9% hadi 4.5% ya kodi ya forodha, ni zana muhimu za kifedha zinazofadhili maboresho endelevu ya miundombinu ya bandari ili kuwa ya kisasa ikiwa ni pamoja na upanuzi wa vituo vya mafuta na mifumo ya usafirishaji mtambuka inayounganisha usafirishaji wa majini na mtandao wa reli na barabara.

“Tanzania tuna MGR, SGR na pia tuna TAZARA. Sasa hizi zote zinatakiwa ziwe zinapokea mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo kuna maendeleo ambayo kwa njia moja au nyingine TPA wanahusika. Haya maendeleo sasa hayawezi kufanyika kama TPA haitakusanya hizi tozo kwa sehemu”, amesema Abel Uronu.

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mawakala wa Meli Tanzania (TASAA), Bw. Abel Uronu