Makubaliano hayo yanatarajiwa kutiwa saini nchini Uswisi na yanaweza kuleta afueni kwa uchumi wa dunia uliotikiswa na vita, ingawa masuala ya nyuklia na vikwazo bado hayajapatiwa suluhisho ya kudumu.
Pakistan imesema Marekani na Iran zimefikia makubaliano ya amani yatakayositisha mara moja operesheni zote za kijeshi, ikiwa ni pamoja na mapigano yanayoendelea nchini Lebanon, hatua inayoweza kuhitimisha vita vilivyodumu kwa zaidi ya miezi mitatu katika Mashariki ya Kati.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye nchi yake imekuwa mmoja wa wapatanishi wakuu katika mzozo huo, amesema makubaliano hayo yatatiwa saini mjini Geneva, Uswisi, baada ya kukamilika kwa mazungumzo ya kiufundi kati ya pande husika.



