Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani imeungana na mikoa mingine kufanya mbio na matembezi ya shukrani kwa walipakodi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 huku ikisisitiza ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati.
Akizungumza baada ya mbio na matembezi hayo yaliyofanyika Juni 27, 2026, Meneja wa TRA Mkoani humo, Peter Eliona, alisema lengo la shughuli hiyo ni kuwashukuru walipakodi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ya sekta ya afya, elimu na miundombinu.
Alieleza maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Miaka 30 ya TRA; Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa kwa Maendeleo na Kujitegemea kwa Taifa Letu,” inayolenga kuhamasisha wananchi kutimiza wajibu wao .
Eliona alieleza ,katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TRA, mamlaka hiyo imeendelea kuboresha huduma kwa kutumia mifumo ya kidijitali, kuimarisha utoaji wa elimu kwa walipakodi na kujenga mazingira rafiki ya ulipaji kodi, hatua zilizochangia kuongeza mapato ya Serikali.
Aidha, aliwahimiza watumishi wa TRA, walipakodi na wananchi kwa ujumla kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuboresha afya zao.
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Lilian Shirima, aliwataka wananchi kuendelea kulipa kodi ili kuimarisha uchumi wa Taifa .
Mbio na matembezi hayo yaliwakutanisha watumishi wa TRA, walipakodi, wadau mbalimbali na wananchi, ikiwa ni sehemu ya shughuli zinazoendelea kufanyika nchi nzima kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya TRA.









