Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia Dodoma
Ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imeanza kuzaa matunda, huku Serikali ikieleza kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya mataifa hayo mawili yatafungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika sekta za nishati, kilimo, usafiri wa anga, utalii, elimu na biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema ziara hiyo imeimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Urusi na kuweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu katika maeneo muhimu ya maendeleo.
Msigwa amesema moja ya mafanikio makubwa ya ziara hiyo ni makubaliano ya kushirikiana katika uzalishaji wa nishati kupitia madini ya uranium yaliyopo nchini, hususan katika eneo la Namtumbo, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika sekta ya nishati.
Katika sekta ya kilimo, amesema Tanzania na Urusi zimekubaliana kushirikiana katika uzalishaji wa ndizi mkoani Morogoro pamoja na uzalishaji wa mbolea, bidhaa ambayo ina mahitaji makubwa ndani na nje ya nchi.
Amesema ushirikiano huo pia utaongeza fursa za biashara na uwekezaji kupitia sekta ya usafiri wa anga, ambapo kuanzia Julai 2, 2026, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linatarajiwa kuanza safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow mara tatu kwa wiki.
“Safari hizi zitafungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi pamoja na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa,” amesema Msigwa.
Katika sekta ya utalii, amesema pande hizo mbili zimekubaliana kushirikiana kuitangaza Tanzania kama kivutio cha watalii kutoka Urusi na mataifa mengine yanayotembelea nchi hiyo.
Aidha, amesema ushirikiano katika elimu utaongezeka kupitia programu za kubadilishana wanafunzi na kuongeza idadi ya nafasi za udhamini kutoka 150 zilizopo sasa hadi zaidi ya 500 kwa Watanzania watakaosomea fani mbalimbali za sayansi nchini Urusi.
Msigwa amesema pia pande hizo zimekubaliana kukuza matumizi ya lugha za mataifa hayo mawili, ambapo Kiswahili kitaendelea kufundishwa nchini Urusi huku Chuo Kikuu cha Dodoma kikitarajiwa kuanza kufundisha lugha ya Kirusi.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanaendana na mkakati wa Serikali wa kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia ushirikiano wa kimataifa unaolenga kuongeza uwekezaji, biashara, ajira na ukuaji wa uchumi.
Mbali na Urusi, Msigwa amesema Tanzania imeendelea kupanua ushirikiano wake na mataifa mengine ikiwemo Singapore na Namibia, huku ikijiandaa kumpokea Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, ambaye atafanya ziara ya kikazi nchini Julai 2 hadi 3 mwaka huu na kushiriki ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Amesema Serikali itaendelea kutumia diplomasia ya uchumi kuvutia mitaji, teknolojia na masoko mapya ili kuchochea maendeleo ya Taifa na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



