Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia , Songea
Kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yatakayofanyika tarehe 1 Julai 2026, TRA Mkoa wa Ruvuma imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ya kivuli na matunda katika hospitali ya wilaya ya Songea mkoani humo.
Maadhimisho hayo yanaambatana na shughuli mbalimbali za kijamii nchini zikiwemo kampeni za mazingira na utoaji wa huduma kwa jamii.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, katibu Tawala wa Wilaya ya Songea Mtela Mwampamba ambaye alimwakilisha mkuu wa Wilaya ya Songea,Kapenjama Ndile alisema kuwa upandaji wa miti unalenga kuchangia uhifadhi wa mazingira, kuboresha mandhari ya kituo cha Afya pamoja na kutoa kivuli na matunda yatakayowanufaisha wagonjwa, wahudumu wa afya na wananchi wanaofika kupata huduma.
Aidha, zoezi hilo linaakisi dhamira ya TRA ya kurejesha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii kupitia shughuli zenye manufaa ya kudumu, sambamba na kuendelea kuhamasisha wananchi kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari ili kuchochea maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, mganga mfawidhi wa hospitali hiyo ya Wilaya ya Songea Dk. John Ndiu ameishukuru TRA Mkoa wa Ruvuma kwa mchango huo, akieleza kuwa miti hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya hospitali na kuongeza ustawi wa mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yamekuwa yakitanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii na mazingira katika maeneo tofauti nchini, zikidhihirisha mchango wa mamlaka hiyo katika maendeleo endelevu pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.



