Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
CHIFU ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wataalamu wa Tiba Asili na Mbadala Mkoa wa Pwani, Salim Mashimba, amesema jamii imeasi na kupuuza mila na desturi za mababu, hali inayotishia ustawi wa maadili na ukuaji wa kizazi kijacho.
Aidha ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuilinda amani na utulivu nchini kwa kuenzi tunu na maadili waliyoachiwa na waasisi wa Taifa.
Chifu Mashimba aliyasema hayo Juni 28,2026 wakati wa kusimika bendera ya asili kwa Daktari Kobelo John huko Zegeleni, Visiga Madafu, Kata ya Visiga, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Alisema ni muhimu jamii kuenzi tamaduni, mila na desturi zake kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Watoto wengi wanakua bila kujengewa misingi ya kutambua mila na desturi za makabila yao, hawajui asili ,matambiko yao , jambo linalowafanya kudharau masuala ya kimila, “Lakini wanapokumbwa na changamoto zinazohitaji maarifa ya asili, ndipo wazazi hukimbilia kwa wazee ama wataalamu wa tiba za jadi,” alisema Chifu Mashimba.
Alimpongeza , Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anawathamini wazee na machifu na anaendelea kufanya kazi kubwa ya kuimarisha uchumi, amani na utulivu nchini.
Hata hivyo aliwataka viongozi wa mikoa na wilaya kushirikiana kwa karibu na machifu na wazee wa kimila.
Pia alikumbusha umuhimu wa kutunza misitu ya asili na kuendelea kupanda miti, akisema baadhi ya miti hiyo ni chanzo cha tiba za asili na inachangia uhifadhi wa mazingira.
Nae Daktari Kobelo John alimshukuru Chifu Mashimba kwa ushirikiano wake na kusisitiza kuwa wataalamu wa tiba za jadi wanapaswa kuzingatia misingi ya taaluma yao bila kujihusisha na ramli chonganishi zinazochochea migogoro katika jamii.
Alisema wataendelea kuelimishana ili kujiepusha na vitendo hivyo na kulinda heshima ya taaluma ya tiba asili.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Zegeleni, Rashid Lukunja, alisema anaheshimu mila, desturi na mizimu ya asili kwa kuwa ni sehemu ya historia, utamaduni na maendeleo ya jamii.




