Serikali imesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya mifugo barani Afrika, hivyo matumizi ya teknolojia ya kisasa ni muhimu katika kulinda mali za wafugaji na kukuza uchumi.
Akizungumza leo Juni 29, 2026, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, amesema uzinduzi wa Smart Mifugo na CRDB Insurance Company kwa kushirikiana na ACRE Africa ni hatua muhimu ya kuimarisha sekta ya mifugo kupitia matumizi ya akili mnemba (AI).
Huduma hiyo ya bima inatumia teknolojia ya AI kutambua mifugo kupitia alama ya pua ya mnyama, hivyo kusaidia kuwalinda wafugaji dhidi ya hasara zinazotokana na vifo vya mifugo, magonjwa na ukame, huku ikipunguza udanganyifu na kurahisisha upatikanaji wa fidia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema teknolojia hiyo itaondoa matumizi ya kupiga chapa mifugo, ambayo huathiri ubora wa ngozi, na kwamba huduma hiyo itapanuliwa pia katika nchi ambazo Benki ya CRDB inafanya shughuli zake, ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava, amewahimiza wafugaji nchini kujisajili kupata huduma hiyo, huku Kamishna wa TIRA, Bagayo Saqware, akisema Smart Mifugo itawawezesha wafugaji kupata fidia kwa haraka pindi wanapokumbwa na majanga kama ukame.




