Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amewataka wataalamu wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kuhakikisha Maonesho ya Nane Nane ya mwaka huu yanakuwa chachu ya kuongeza tija, uzalishaji na thamani ya mazao ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kunenge ametoa kauli hiyo katika Ukumbi wa JKT mkoani Morogoro wakati akifungua kikao cha pili cha maandalizi ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki, kilichowakutanisha wakuu wa wilaya, Katibu Tawala wa Kanda ya Mashariki, wakuu wa idara za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na maofisa habari.

Alisema maonesho hayo yanapaswa kuwa jukwaa la kutafuta na kuwasilisha suluhisho la changamoto zinazowakabili wakulima, wafugaji na wavuvi, badala ya kuishia kuonesha bidhaa na teknolojia zisizoleta mchango wa moja kwa moja katika kuongeza uzalishaji.

Alieleza kuwa, Serikali imelenga kukuza sekta ya kilimo kwa kufikia ukuaji wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hivyo wataalamu wanapaswa kuandaa mikakati yenye viashiria na takwimu sahihi zitakazowezesha kupima na kufuatilia utekelezaji wa malengo hayo katika ngazi za mikoa na kanda.

Aidha Kunenge, alitoa rai kwa wataalamu kuhakikisha maonesho hayo yanaonesha teknolojia na ubunifu unaowawezesha wakulima kuongeza uzalishaji, kudhibiti magonjwa ya mazao na mifugo, pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kunenge alisema Tanzania ina dhamira ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula barani Afrika, jambo linalohitaji kuungwa mkono kwa vitendo kupitia uwekezaji katika kilimo cha kibiashara na uzalishaji wa mazao yenye soko la uhakika.

Vilevile, alifafanua Serikali imeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za mifugo na kusisitiza matumizi bora ya rasilimali hizo ili kuongeza mchango wa sekta za mifugo na uvuvi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.