Na. Catherine Sungura
Uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuikabidhi Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) jukumu la kujenga miundombinu ya barabara za maingilio kwenye uwanja wa utakaotumika wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) jijini Arusha ni uthibitisho wa imani kubwa iliyonayo kwa taasisi hiyo katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Taifa.
Kwa miaka kadhaa sasa TARURA imeendelea kuonesha uwezo mkubwa wa kusimamia na kutekeleza miradi ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini, ikiboresha miundombinu inayochochea ukuaji wa uchumi, biashara, utalii na huduma za kijamii. Kutokana na rekodi hiyo ya mafanikio si jambo la kushangaza kuona serikali ikiendelea kuiamini katika miradi yenye hadhi ya kimataifa kama maandalizi ya AFCON.
AFCON si mashindano ya mpira wa miguu pekee, bali ni jukwaa la kutangaza Tanzania duniani. Mafanikio ya mashindano hayo yanategemea pia ubora wa miundombinu ya usafiri inayorahisisha wageni, timu, viongozi na watalii kufika katika maeneo mbalimbali kwa urahisi na usalama.
Hivyo, ujenzi wa barabara za kisasa zinazounganisha viwanja na maeneo mengine muhimu ni sehemu muhimu ya maandalizi hayo.
Kukabidhiwa kwa mradi huu kunatoa fursa kwa TARURA kuonesha zaidi uwezo wake wa kitaalamu katika utekelezaji wa miradi mikubwa. Aidha, ni nafasi ya kuongeza uzoefu katika kusimamia miradi inayohitaji viwango vya juu vya ubora na utekelezaji kwa wakati maalumu kutokana na ratiba za mashindano ya kimataifa.
Jambo jingine muhimu ni matumizi ya mfumo wa “Sanifu na Jenga” (Design and Build) unaotumika katika mradi huu.
Mfumo huu una faida nyingi ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa miradi, kupunguza urasimu wa hatua nyingi za zabuni, kuongeza uwajibikaji kwa mkandarasi mmoja anayehusika na usanifu pamoja na ujenzi na kuhakikisha ubora wa kazi unaendana na mahitaji yaliyokusudiwa.
Kupitia mfumo huo, TARURA inapata nafasi ya kujifunza na kuimarisha zaidi uwezo wake wa usimamizi wa miradi ya kisasa, jambo ambalo litakuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo nchini siku zijazo.
Hii inaendana na dhamira ya serikali ya kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa ufanisi, ubora na kwa thamani halisi ya fedha za umma.
Kwa upande wa uchumi, barabara zitakazojengwa hazitakuwa na manufaa wakati wa AFCON pekee. Miundombinu hiyo itaendelea kutumiwa na wananchi wa Arusha kwa miaka mingi baada ya mashindano kumalizika. Hivyo, uwekezaji huu utachochea biashara, utalii, uwekezaji na usafirishaji wa bidhaa na huduma katika jiji hilo na maeneo jirani.
Kwa ujumla, kuaminiwa kwa TARURA kutekeleza mradi wa barabara za kuingia kwenye maeneo ya AFCON Arusha ni matokeo ya utendaji wake mzuri na uwezo wake uliothibitishwa. Ni hatua inayodhihirisha imani ya serikali kwa taasisi za ndani na uwezo wa wataalamu wa Kitanzania katika kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya taifa.
Mradi huu utakapokamilika utaongeza hadhi ya TARURA na kuifanya kuwa miongoni mwa taasisi muhimu zaidi katika maendeleo ya miundombinu nchini.


