Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es Salaam

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limefanikiwa kubuni dawa ya asili ya kuchakata ngozi inayotokana na mimea, hatua inayotarajiwa kupunguza matumizi ya kemikali za viwandani, kulinda afya za watumiaji na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 3, 2026, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia za Nguo na Ngozi wa TIRDO, Mhandisi na Mtafiti Yusufu Sampuli, amesema lengo la shirika kwa mwaka huu ni kuhamasisha matumizi ya teknolojia za asili badala ya kemikali katika uchakataji wa ngozi.

Alisema dunia kwa sasa inaelekeza nguvu katika matumizi ya bidhaa rafiki kwa mazingira na afya, jambo ambalo limeongeza mahitaji ya bidhaa zinazochakatwa kwa kutumia malighafi za asili, hususan katika soko la kimataifa.

“Wananchi wanapaswa kufahamu kuwa dunia inapambana kulinda mazingira na afya za wafanyakazi pamoja na watumiaji wa bidhaa mbalimbali. Hivi sasa soko la bidhaa zilizochakatwa kwa kutumia vitu vya asili limeongezeka kwa kiasi kikubwa. Ukitazama soko la Ulaya, kuna mahitaji makubwa ya ngozi zilizochakatwa kwa kutumia mimea kuliko zile zinazotumia kemikali ambazo zina madhara kwa afya na mazingira,” amesema Sampuli.

Aliongeza kuwa baada ya mafanikio ya ubunifu huo, baadhi ya wajasiriamali wa mkoa wa Kilimanjaro tayari wameanza kutumia dawa hiyo katika uchakataji wa ngozi na kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Sampuli alisema TIRDO inaendelea kuwafuatilia na kuwapa ushauri wa kitaalamu wajasiriamali hao ili kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa ufanisi na kuwasaidia kuzalisha bidhaa zenye ushindani ndani na nje ya nchi.

Aidha, alisema dawa hiyo ya asili inapatikana kupitia TIRDO, ambapo wananchi na wadau wanaweza kupata taarifa zaidi kupitia tovuti na namba rasmi za ofisi za shirika.