Na DK Reuben Lumbagala

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anatambulika kimataifa katika nyanja mbalimbali kutokana na utendajikazi wake uliotukuka. Miongoni mwa maeneo yanayomtambulisha kwa upekee ni pamoja na kuwa Kinara wa Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto barani Afrika.

Ni heshima ya kipekee aliyoipata kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya, ambapo matunda yake yameonekana hasa katika kupungua kwa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Kwa wadhifa huu, Rais Dk. Samia anao wajibu wa kuhakikisha nchi zote 54 za barani Afrika na Tanzania ikiwemo, zinaendea kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kiwango kikubwa.

Hii inatokana na ukweli kuwa, kundi la mama na mtoto ni wadau muhimu katika juhudi za maendeleo. Ni kundi ambalo linapaswa kuhakikishiwa usalama wa maisha na kamwe uzazi usio tishio la usalama wao.

Juhudi za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa sehemu kubwa zinahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali hasa katika kubadilishana uzoefu, teknolojia na uwekezaji wa miundombinu bora ya afya na vifaa tiba vya kisasa.

Kwa kutumia ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi (Public and Private Partnership – PPP), juhudi na mapambano ya kupunguza vifo vya mama na mtoto zitafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Ili jambo hili liwe halisi, Julai 02, 2026, Rais Dk. Samia alifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Sera, Uhusiano na Ushirikiano na Serikali (PGRP), Divisheni ya Afrika na India kutoka Taasisi ya Gates, Bi. Caty Fall Sow ambaye aliambatana na ujumbe wake, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Haya yamefanyika ikiwa ni mwendelezo wa harakati chanya za uboreshaji wa afya ya uzazi ya mama na mtoto Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Bi. Sow alimpongeza Rais Samia kwa kuteuliwa kwake kuwa Bingwa wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama, Mtoto Mchanga na Mtoto, na akathibitisha upya dhamira ya Taasisi ya Gates ya kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na Waafrika za kumaliza vifo vinavyoweza kuzuilika vya akina mama na watoto,” ilieleza Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.

Aidha, taarifa imesisitiza kuwa pande zote mbili zimejadili namna ya kuimarisha ushirikiano zaidi katika maeneo ya afya ya mama na mtoto, chanjo, lishe, kuimarisha mifumo ya huduma na kudhibiti magonjwa.

Naye, Rais Dk. Samia amesema, “Dhamira yetu ni kuhakikisha kila mama na kila mtoto anapata huduma bora za afya na nafasi ya kuishi maisha yenye afya na matumaini”.

Taasisi ya Gates ni mdau mkubwa wa uimarishaji wa masuala ya afya barani Afrika, jambo linalosaidia kuimarika kwa huduma za afya na kuwezesha kufanikiwa kwa mipango ya serikali ya kuwahudumia wananchi wake.

Kutokana na kazi kubwa aliyonayo Rais Dk. Samia ya kusaidia mafanikio ya masuala ya afya ya uzazi ya mama na mtoto barani Afrika, Juni 02, 2026, alimteua Bi. Ummy Mwalimu kuwa Mshauri wa Rais – Masuala ya Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto.

Maoni: 0620 800 462.