Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kushuhudia hafla ya uwasilishaji Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar, itakayofanyika tarehe 09 Julai 2026, saa 4.00 asubuhi, katika viwanja vya Ikulu, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi, Mawasiliano, Ikulu Zanzibar Raqey Mohamed, imesema Hafla hiyo inalenga kuwasilisha Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama Cha Mapinduzi na ACT-Wazalendo, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha maridhiano, mshikamano, utulivu wa kisiasa, amani na ustawi wa Zanzibar.

Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi, pamoja na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Mhe. Othman Masoud Othman, watasıkiliza uwasilishaji wa Tamko la Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Taasisi za Kiraia na Waandishi wa Habari.

Hafla hiyo itarushwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na mitandao ya kijamii, kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa.