Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesaini kuwa sheria muswada unaoongeza muda wake wa kuhudumu madarakani kwa miaka miwili zaidi, hadi mwaka 2030, msemaji wa serikali Nick Mangwana amesema Jumanne.

Mwezi uliopita, mabunge yote mawili ya Zimbabwe yaliidhinisha muswada huo.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Mangwana alisema: “Imesainiwa, imethibitishwa na sasa ni sheria,” akiambatanisha nakala ya sheria hiyo.

Sheria hiyo pia ina kipengele kinachoruhusu rais kuchaguliwa na Bunge badala ya kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi kupitia kura.

Dalili kwamba Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, alitaka kuendelea kubaki madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili mwaka 2028 zilianza kujitokeza takribani miaka miwili iliyopita.

Wafuasi wake walianza kuimba kaulimbiu katika mikutano ya chama tawala ZANU–PF wakimtaka apewe muda zaidi ili akamilishe ajenda yake ya maendeleo.

Mwaka uliopita, chama cha ZANU–PF kilipitisha azimio la kufanya marekebisho ya katiba ili kuongeza muda wa mihula ya urais. Pendekezo hilo lilipata idhini ya Baraza la Mawaziri mwezi Februari.