Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza mageuzi makubwa ya sekta ya elimu kwa kupitia upya kozi na programu za mafunzo ili ziendane na mahitaji halisi ya jamii, soko la ajira na mabadiliko ya uchumi wa kisasa, hatua inayolenga kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana ndani na nje ya nchi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Caroline Nombo, amesema hatua hiyo imechochewa na hitaji la kuwa na mfumo wa elimu unaokwenda sambamba na mabadiliko ya wakati, akibainisha kuwa mjadala unaoendelea katika mitandao ya kijamii kuhusu kozi zinazofaa kusomwa na wahitimu wa kidato cha sita umeonyesha wazi umuhimu wa kufanya maboresho hayo.
Akizungumza Julai 13, 2026, wakati wa kufungua Kikao cha Mwaka cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Profesa Nombo amesema mrejesho huo umeifanya wizara kujitathmini upya ili kuhakikisha mitaala na programu za elimu zinazalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
“Mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya elimu yanapaswa kuwa chachu ya kuharakisha mageuzi yanayolenga kuandaa rasilimali watu itakayokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa,”ameeleza Prof.Nombo
Amesema mkakati mpya wa wizara unajumuisha maboresho ya mitaala, matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uwekezaji wa elimu pamoja na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya kupanga na kufanya maamuzi.
“Mrejesho tunaoupata unatufanya tujitathmini na kuangalia aina ya kozi tunazotoa. Tunahitaji kuongeza ubunifu na unyumbufu katika kuwapa wanafunzi fursa ya kusoma taaluma zinazojibu mahitaji ya maendeleo ya taifa,” amesema.
Profesa Nombo amesema sekta ya elimu ndiyo msingi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo ni muhimu mipango yote ya wizara ikaendana na matarajio ya taifa ya kujenga uchumi unaotegemea maarifa, sayansi na teknolojia.
“Tumekutana kufanya tathmini ya tulikotoka, tulipo na tunapokwenda. Ni wajibu wetu kuhakikisha sekta ya elimu inatoa mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.
Aidha, ameagiza taasisi zote zilizo chini ya wizara kuhakikisha mifumo yao ya TEHAMA inaunganishwa na Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Elimu (ESMIS) ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa takwimu na kurahisisha maamuzi ya kisera.
Amesema hatua hiyo pia inatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana na kufanya kazi kwa pamoja.
Katibu Mkuu huyo pia amesisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa elimu ili kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha miundombinu na kupanua fursa za kujifunza kwa Watanzania wengi zaidi.
Amesema pamoja na kuendelea kuboresha mitaala, wizara itaweka mkazo katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili wahitimu wawe na maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya taifa na dunia.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Daniel Mushi, amewataka viongozi wa taasisi mbalimbali kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mafanikio yanayopatikana kupitia utekelezaji wa miradi na programu za Serikali katika sekta ya elimu.
Katika kikao hicho, viongozi wa wizara, wakurugenzi, wakuu wa vitengo na wakuu wa taasisi walijadili nafasi ya elimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, mfumo wa ESMIS, Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 pamoja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.





