Mkutano wa 28 wa Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ngazi ya wataalamu umefunguliwa leo Julai 13, 2026, mjini Salima, Malawi ambapo wajumbe watajadili agenda mbalimbali, zinazolenga kuimarisha ulinzi na usalama, demokrasiaa na utawala bora kwenye kanda ya SADC.

Ujumbe wa Tanzania katika ngazi hiyo unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ambaye ameambatana na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi na wawakilishi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwemo Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi, Luteni Generali Salum Haji Othman.

Agenda zitakazojadiliwa ni pamoja na taarifa ya hali ya kisiasa na usalama hususan Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Madagascar na Msumbiji kwenye jimbo la Cabo Delgado.

Aidha, wajumbe watapitia utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na usambazaji wa machapisho ya Brigedia Generali Hashim Mbita yaliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kwenye nchi wanachama, utayarishaji wa makala mjongeo ya Brigedia Generali Hashim Mbita na kuenzi historia ya waasisi wa SADC ambapo shughuli mbalimbali zinakusudiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kujenga makumbusho na uandaaji wa Makala mjongeo ambazo pamoja na mambo mengine zinalenga kuhifadhi historia hiyo adhimu na kuirithisha kwa vizazi vya sasa na vinavyokuja katika nchi za SADC na duniani kwa ujumla.

Tanzania pia itashiriki kikamilifu katika mkutano wa ngazi ya Mawaziri ambao utafanyika Julai 16 na 17, 2026 mjini Salima.