Na OWM–TAMISEMI, Sumbawanga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amempongeza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Mhe. Jacqueline Mzindakaya, kwa juhudi zake za kuwaunganisha wadau mbalimbali, ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, uongozi wa mkoa wa Rukwa na halmashauri zake, hatua iliyowezesha kufanyika kwa mafunzo ya utoaji elimu kuhusu fursa za mitaji na huduma za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi mkoani Rukwa.

Prof. Shemdoe ametoa pongezi hizo Julai 13, 2026 katika Ukumbi wa Country Hotel mjini Sumbawanga wakati akifungua mafunzo ya utoaji elimu kuhusu fursa za mitaji na huduma za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, mafunzo ambayo yameratibiwa na Mbunge huyo kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Prof. Shemdoe amesema kuwa, anaamini mafunzo hayo yatafungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa, akiwataka washiriki kutumia elimu watakayopata kuanzisha biashara mpya, kuimarisha biashara walizonazo, kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa na mazao wanayozalisha, na kuongeza kwamba mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwafikia wananchi wa makundi yote, wakiwemo watu wenye ulemavu.

Aidha, Prof. Shemdoe amezielekeza ofisi za mikoa na halmashauri nchini kutenga nafasi za ofisi kwa ajili ya vituo vya uwezeshaji kiuchumi vitakavyohudumia vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na makundi mengine maalum yanayojishughulisha na kilimo, ufugaji, uvuvi, umachinga, bodaboda, ufundi na ujasiriamali, ili kujenga taifa lenye uchumi imara, shindani na jumuishi.

“Ninazielekeza ofisi zote za mikoa na halmashauri nchini kuiga mfano wa mkoa wa Rukwa kwa kutenga ofisi za vituo vya uwezeshaji kiuchumi, vitakavyowawezesha wananchi kupata taarifa, ushauri na kuunganishwa na fursa za mitaji na huduma za uwezeshaji ili wananchi wajikwamue kiuchumi,” amesema Prof. Shemdoe.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere, amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kukubali kumwakilisha Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika ufunguzi wa mafunzo hayo, akisema uwepo wake unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha kiuchumi vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na makundi mengine maalum.

Kwa upande wake, Mhe. Mzindakaya amesema uwepo wa Prof. Shemdoe akimuwakilisha Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika ufunguzi wa mafunzo hayo, ni ishara ya namna Serikali inavyothamini jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bw. Gwakisa Bapala, amesema mafunzo hayo yatawawezesha wananchi kunufaika na huduma za mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji kwa ajili ya kuanzisha miradi mipya, kukuza biashara zilizopo, kuongeza thamani ya mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa na Taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo yanayofanyika katika halmashauri zote nne za mkoa wa Rukwa kuanzia Julai 13 hadi 16, 2026, yamelenga kuwafikia wananchi zaidi ya 1,000 na kuwapa maarifa yatakayowawezesha kutumia kikamilifu fursa za mitaji na huduma za uwezeshaji kwa maendeleo yao na ya Taifa, fursa ambazo zinatoka katika mifuko na taasisi 15 ikijumuisha NMB, CRDB, Azania Bank, TADB, AGITF, Self MF, BOT, Machinga Fund, YDF, SIDO, Pass Trust, Pass Leasing, EFTA, TaFF na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa.