NA JOE BEDA RUPIA
“Utakitoaje kibanzi ndani ya jicho la mwenzako nawe lako lina boriti ndani yake?” Swali la Yesu Kristo ndani ya Biblia. Linafikirisha sana. Linatafakarisha pia.
Hili nimelifikiria wiki hii kutokana na hali inayoendelea ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini; Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa miaka mingi sasa, CHADEMA imejijengea taswira ya kuwa sauti kuu ya ukosoaji dhidi ya serikali na taasisi za umma, na hili ni jambo jema sana.
Kimekuwa chama kinachouliza maswali magumu kuhusu matumizi ya fedha za umma, uwajibikaji wa viongozi, rushwa, ubadhirifu na maadili katika uongozi wa kila ngazi nchini.
Katika mfumo wa kidemokrasia, nafasi hiyo ni muhimu sana. Taifa lolote linalotaka kukua kidemokrasia linahitaji chama cha upinzani chenye nguvu, chenye uwezo wa kuhoji, kukosoa na kusukuma mageuzi pale panapohitajika. Kwa kiasi kikubwa, CHADEMA imekuwa ikifanya kazi hiyo vema kwa miaka kadhaa.
Lakini kuna kanuni moja ambayo haiwezi kuepukwa katika hali ya kibinadamu, kwamba anayekosoa wengine lazima naye awe tayari kukosolewa.
Ndiyo maana tuhuma zinazomkabili Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Tanzania Bara), John Heche, zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa, si kwa sababu tu zinamhusu kiongozi mmoja, bali kwa sababu zinagusa moja kwa moja suala la uadilifu wa taasisi nzima.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoibuka kutoka ndani ya vikao vya chama vilivyofanyika mkoani Kigoma, Heche anatuhumiwa kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali na kutowasilisha fedha hizo kwa utaratibu unaotambulika ndani ya chama.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo Godbless Lema na Joseph Mbilinyi (Sugu), wamezungumzia hadharani madai yanayodaiwa kujadiliwa katika Kamati Kuu ya chama.
Ni muhimu kusisitiza kuwa haya bado ni madai ambayo yanahitaji maelezo ya wazi na ya kina kutoka kwa wahusika. Katika mazingira ya kawaida ya taasisi yoyote inayojali uwazi na uwajibikaji, tuhuma za namna hii haziwezi kuachwa zikining’inia bila majibu yanayoeleweka.
Tatizo hapa si tuhuma zenyewe. Tatizo kubwa zaidi ni namna ambavyo sehemu ya jamii imekuwa ikiitazama CHADEMA kwa miaka mingi.
Kuna wakati chama hicho kimekuwa kama mtoto anayedekezwa! Kimekuwa kikitazamwa kwa huruma kiasi kwamba baadhi ya watu wanaogopa hata kukikosoa pale kinapokosea.
Makosa ambayo yangezua mjadala mkubwa kama yangetokea serikalini au katika chama kingine, mara nyingi hupokewa kwa tahadhari kubwa yanapohusu CHADEMA.
Wapo wanaoamini kuwa kwa sababu chama hicho kimepitia vipindi vigumu vya kisiasa, basi hakipaswi kukosolewa sana. Wengine huona kuwa kila ukosoaji dhidi ya chama hicho ni sehemu ya njama za kisiasa. Matokeo yake, wakati mwingine hoja halali za uwajibikaji hufunikwa na mihemko ya kisiasa.
Lakini huo si msingi mzuri wa kujenga taasisi imara! Demokrasia haihitaji taasisi zinazolindwa dhidi ya ukosoaji. Inahitaji taasisi zinazoweza kuhimili ukosoaji.
Ikiwa chama kinadai uwazi na uwajibikaji serikalini, basi wananchi wana haki ya kudai uwazi na uwajibikaji wa aina hiyo hiyo kutoka ndani ya chama.
Ikiwa chama kinataka viongozi wa umma waeleze walivyotumia fedha za wananchi, basi viongozi wake nao wanapaswa kuwa tayari kueleza walivyoshughulikia fedha za chama!
Katika mjadala huu, jambo moja limezua maswali mengi zaidi. Kumekuwa na taarifa kwamba CHADEMA imeamua kubadili mfumo wa ukusanyaji wa michango ili fedha zielekezwe moja kwa moja makao makuu ya chama badala ya kupitia kwa viongozi binafsi.
Kwa nini mfumo ubadilishwe? Mara nyingi taasisi hubadili mifumo pale zinapogundua udhaifu, mkanganyiko wa kiutendaji au mianya inayoweza kusababisha malalamiko.
Hivyo, hatua ya kupeleka michango moja kwa moja makao makuu ni ishara ya kuwapo tatizo katika mfumo wa awali. Ni ishara ya kuwapo ukweli wa upigaji ndani ya chama.
Kwa kawaida, taasisi zinazokua hujengwa juu ya mifumo, si juu ya watu. Fedha za chama hazipaswi kutegemea uaminifu wa mtu mmoja mmoja, hata kama mtu huyo ni kiongozi mkubwa kiasi gani.
Zinapaswa kulindwa na taratibu, kanuni na mifumo inayoweza kukaguliwa na kuthibitishwa wakati wowote. Hili ni somo ambalo vyama vyote vya siasa vinapaswa kujifunza.
Kuna wanaosema mjadala huu ulipaswa kubaki ndani ya vikao vya chama. Hoja hiyo ina mantiki yake. Hakuna taasisi inayopenda migogoro yake ya ndani kuwa habari kwa umma!
Lakini ukweli ni kwamba mara tu tuhuma zinapohusu fedha za chama, na hasa pale viongozi wa juu wanapozungumza hadharani, suala hilo linaacha kuwa la ndani. Linakuwa suala la uaminifu kwa umma.
Vyama vya siasa haviishi kwa wanachama pekee. Vinaishi kwa imani ya wananchi. Vinaishi kwa michango ya wanachama na wadau. Vinaishi kwa taswira vinayojijengea mbele ya umma. Na imani hiyo hujengwa kwa uwazi.
Hakuna anayefaidika CHADEMA ikidhoofika. Hakuna anayefaidika taasisi za upinzani zikikosa nguvu. Lakini hakuna anayefaidika pia pale taasisi hizo zinapoonekana kuwa na vipimo viwili tofauti vya maadili – kimoja kwa serikali na kingine kwao wenyewe.
Mamlaka ya kukosoa wengine hutokana na mfano unaouonyesha wewe mwenyewe.
Chama kinapopaza sauti dhidi ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka au ubadhirifu wa fedha za umma, wananchi hutegemea kuona viwango vya juu zaidi vya uwajibikaji ndani ya chama hicho kuliko hata vinavyodaiwa kwa wapinzani wake.
Hicho ndicho kinachoitwa ‘moral authority’ ya kumwambia mwingine afanye jambo kwa sababu wewe mwenyewe unalifanya.
Historia ya siasa duniani inaonyesha kuwa vyama vingi vilianza kudhoofika pale viliposhindwa kuishi kwa misingi vilivyokuwa vinaihubiri.
Sasa, jambo la msingi kwa CHADEMA ni kumuwajibisha yeyote aliyekosea, hivyo kujijengea heshima kwa umma.
Nguvu ya taasisi hujidhihirisha pale inapokabiliwa na tuhuma, ikazichunguza kwa haki, ikawawajibisha wahusika kisha ikatoka ikiwa imara zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Niseme neno moja tu kwa CHADEMA; kabla ya kukosoa wengine, jisafisheni wenyewe. Ondoeni boriti kwenye jicho lenu ili muweze kuondoa kibanzi kwenye jicho la serikali.

